LEO nimekuwa na wakati mzuri sana katika usomaji wa vitabu. Nimevisoma vitabu viwili vya Nguli katika riwaya za kijasusi, Aristablus Elvis Musiba. Nilianza na Kufa na Kupona. Hofu ikafuatia.
Kufa na Kupona, ndicho kitabu cha kwanza kabisa cha kijasusi mimi kuwahi kukisoma katika maisha yangu. Nikiwa mdogo, nyumbani kwetu kulikuwepo kitabu hicho. Nilikipenda sana. Sikumbuki nilikuwa nimekisoma mara ngapi hadi tu kufikia Darasa la Tatu.
Tangia hapo, nikaondokea kuwa shabiki mkubwa sana wa kazi za Nguli Musiba. Uandishi wake ulinifanya niwe shabiki mkubwa wa Willy Gamba.
Baadaye kidogo, nikiwa Darasa la Nne, nilikuwa tayari nimemsoma Nguli Musiba kwenye Kikomo, Kikosi cha Kisasi na Njama. Nikiwa Kidato cha Kwanza, ndipo nikamsoma kwenye Hofu.
Baada ya hapo, sikuwahi kukutana na kitabu chake chochote, hadi mwaka jana; kwa hisani ya rafiki yangu, nilipomsoma kwenye Uchu.
Tangu zamani, nadhani hadi nilipoanza Kidato cha Kwanza, nilisadiki ya kwamba, Willy Gamba ni kiumbe hai. Namna Nguli Musiba alivyobarikiwa ufundi wa kusimulia, kumhusu mpelelezi huyu nambari moja barani Afrika, iliniwia vigumu hata kudhani tu, eti ni mtu wa kufikirika.
Namna Nguli Musiba alivyomwelezea, mwenyewe alijulia vema kuteka nadhari ya msomaji. Kwa mfano, kwenye Hofu, Nguli Musiba anaandika:
"Willy Gamba alikuwa ni mpelelezi maarufu aliyekuwa akifanya kazi katika Idara ya Upelelezi ya Tanzania. Sifa zake zilitapakaa katika bara zima la Afrika. Kutokana na ujasiri wake, watu wengi walifikiri mtu huyu alikuwa wa kubuniwa tu, maana watu walifikiri kuwa vitendo vya Willy Gamba vilikuwa kama mchezo wa sinema.
Lakini ukweli ni kwamba, mtu huyu yupo na vitendo vyake ni vya kweli tupu."
Waama, niliyasadiki maneno haya.
Nguli Musiba ni miongoni mwa waandishi waliochangia kwa kiasi kikubwa sana kunichochea hamu ya kupenda kuandika riwaya. Tena, riwaya za kijasusi. Ingawa, hadi sasa, bado sijachapa riwaya ya aina hiyo hata moja, bado ninayo kiu kubwa sana ya kuandika hivyo.
Tukirejea kwa Nguli Musiba, mambo yaliyonivutia leo hii wakati nikisoma riwaya hizi mbili, ni mengi. Lakini jambo kubwa ukiachilia mbali umahiri wa usimuliaji, ni utajiri wa maarifa kwa mwandishi.
Riwaya hizi zote mbili, zinagusa hujuma za makaburu, wakati wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Hujuma hizi, zilizilenga nchi zilizokuwa mstari wa mbele (makaburu waliziita viherehere) katika kuwasaidia wapigania uhuru Kusini mwa Afrika. Hususani, Msumbiji, Zimbabwe, Angola na Namibia.
Nguli Musiba alizielewa kwa kina siasa za kupigania uhuru. Bila shaka alikuwa msomaji mzuri sana na mfuatiliaji mkubwa wa mambo. Hata leo hii unapomsoma, unapata ile ladha hasa ya mwandishi mwenye kuwa na maarifa makubwa juu ya suala analolisimulia.
Jambo jingine linalosisimua kwenye riwaya za Willy Gamba, ni mpangilio wa visa. Kuna nyakati unasoma roho juu juu ukidhani Willy atauawa. Halafu, Willy hajawahi kukumbana na 'hapana' pale macho yake yanapoona.
Ama hakika, Jumapili yangu imekuwa muruwa kabisa.
Alamsiki.
Fadhy Mtanga,
Iringa, Tanzania.
Jumapili, Januari 28, 2018.