Quantcast
Channel: Fadhy Mtanga
Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Faida za kusoma vitabu

$
0
0



TAREHE kama ya leo mwaka jana, niliweka bandiko kwenye ukuta wangu wa Facebook, nikielezea faida za kusoma vitabu. Kwa kuwa, tumo tu mwanzoni mwaka wa 2018, nimeona si vibaya nikiikumbusha jamii juu ya umuhimu wa kusoma vitabu.

Pengine, na ningetamani iwe hivyo, andiko hili linaweza kuchochea hamu ya usomaji vitabu miongoni mwetu.

Wakati fulani, unaweza kujiuliza, kwa nini watu wanapenda sana kusoma vitabu? Kwa nini watu wanaweka malengo ya usomaji wa vitabu? Zipo faida nyingi mno. Faida chungu-mbovu za usomaji wa vitabu.

Mwanzoni mwa mwaka jana, katika pitapita yangu mitandaoni, nilikutana na faida lukuki za usomaji vitabu. Miongoni mwa faida hizo, nilivutiwa zaidi na faida 10 zilizobainishwa na mwandishi Lana Winter-Hébert, kama alivyoyaandika kwenye mtandao wa Lifehack.

Mwandishi anasema ni vema kusoma vitabu kila siku kwa kuwa kuna faida zifuatazo:

1. Kuongeza uwezo wa ubongo
Kwamba, kama ambavyo kazi ama mazoezi huongeza uwezo wa misuli ya mwili, basi, ndivyo hivyo kusoma huongeza uwezo wa ubongo katika kufanya kazi. Uwezo wa ubongo unapokuwa umeongezeka, ndivyo msomaji wa vitabu anavyopunguza hatari ya kushambuliwa na maradhi ya Alzheimer na Dementia, kwa kuwa kuufanya ubongo wako kuwa thabiti kunaufanya kutopoteza uwezo wake.

2. Kupunguza msongo wa mawazo
Haijalishi unapitia magumu yepi mahala pa kazi, ama migogoro mikubwa kiasi gani katika mahusiano ama masahibu yasiyohesabika katika maisha yako ya kila siku; hayo yote hupunguza kukuzonga kadri unavyozama katika kusoma simulizi kabambe inayokusisimua hasa. Riwaya iliyoandikwa kiustadi, huweza kukusafirisha hadi katika ulimwengu mwingine kabisa na kukuondoa katika hali ya sasa ikuzongayo hivyo kukupa nafasi ya kuburudika kiakili.

3. Kuongeza maarifa
Kila jambo unalolisoma hukupa taarifa mpya. Huwezi fahamu ni wakati gani maarifa hayo yatakusaidia katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha yako. Kuwa na utajiri wa maarifa ni nyenzo muhimu sana ya kukabiliana na changamoto pindi zinapojitokeza maishani mwako. Kumbuka kwamba, katika maisha, unaweza kupoteza vitu vingi; kazi, cheo, pesa, marafiki, hata afya yako - lakini, huwezi kuyapoteza maarifa uliyonayo.

4. Kuongeza ukwasi wa misamiati
Kadri unavyosoma vitabu vingi kutoka kwa waandishi mbalimbali, ndivyo unavyojitajirisha juu ya misamiati. Kuwa na ukwasi wa misamiati husaidia sana katika maisha ya kila siku. Huongeza kujiamini na uwezo wa kuzungumza mbele ya hadhira. Hadhira yoyote huvutiwa zaidi na mzungumzaji mwenye kujiamini na mwenye uwezo wa kucheza na misamiati ya lugha kwa umaridadi kadri ya muktadha.

5. Kuongeza uwezo wa kutunza kumbukumbu
Pindi usomapo kitabu, kuna mambo kadha wa kadha hujikuta ukiyakumbuka kutokana na kitabu ulichokisoma. Mambo hayo yanaweza kuwa juu ya wahusika, historia zao, michakato yao katika mapambano kwenye maisha na mengineyo mengi. Ubongo wa binadamu ni kitu cha ajabu sana. Kadri ubongo wako unavyoyakumbuka mambo hayo, ndivyo uwezo wake binafsi wa kutunza kumbukumbu hata kwa mambo mengi mengine unavyoongezeka.

6. Uwezo mkubwa wa kufikiria na kupambanua mambo
Umewahi kusoma riwaya kwa mfano, ukakutana na kadhia kubwa inayowazonga wahusika wa riwaya hiyo, halafu ukawa unafikiria namna za utatuzi kabla hata hujafahamu mwandishi ametatua vipi? Bila shaka, wasomaji wengi hukutana na hali hii.

Hii huashiria kuongezeka kwa uwezo wako wa kutatua mitanzuko katika maisha ya kila siku. Kuongezeka kwa uwezo huo huleta usaidizi wa msingi pindi unapokabiliana na kadhia nyingine yoyote katika maisha yako. Lakini pia, kuongeza uwezo wa kuwasaidia watu wengine wanaokuzunguka katika kubaliana na masahibu yanayoondokea kuwazonga.

7. Kuongeza uwezo wa kuzingatia mambo
Kwenye dunia yetu ya sasa iliyotekwa na mambo ya intaneti, uwezo wa watu kuzingatia mambo umepungua kwa kiasi kikubwa sana. Ndani ya dakika 5 tu kwa mfano, mtu mmoja anaweza kujikuta kadonoadonoa kwenye barua-pepe, wasapu, twita, instagramu, fesibuku, skaipu na kwingineko. Kupoteza uzingativu huathiri wa mtu kufanya kazi na kuleta matokea yanayotarajiwa.

Lakini, unaposoma kitabu, nadhari yako yote huhamia kitabuni. Hivyo, hali hivyo huongeza uwezo wako wa kuzingatia jambo unalolifanya pasipo kuruhusu mambo mengine kuathiri. Unapotumia walau dakika 15 hadi 20 kila siku kusoma kitabu kabla hujaanza kazi asubuhi, kunaongeza uwezo wako wa kuizingatia kazi yako pindi uanzapo kuifanya.

8. Kuboresha stadi za uandishi
Awali imesemwa namna kusoma vitabu kunavyochochea ukwasi wa misamiati. Kwa nyongeza, kusoma vitabu huboresha stadi za uandishi. Unaposoma vitabu kutoka kwa waandishi mbalimbali ambao wametumia weledi na mbinu kadha wa kadha, unaongeza ustadi wako binafsi katika uandishi. Daima, waandishi mahiri ni wale waliopata msukumo kutokana na usomaji wa kazi za waandishi wengine, hususani, wabobevu.

Ni kama vile tu ilivyo kwa mwanamuziki. Mwanamuziki mahiri ni yule aliye fundi wa kusikiliza kazi za wanamuziki wengine.

9. Huchochea utulivu
Kusoma vitabu huleta raha! Unaposoma kitabu kizuri, kile unachokisoma huleta hisia za amani na utulivu moyoni mwako. Kusoma maandiko ya kiroho hupunguza shinikizo la damu na kuleta kiwango cha juu cha utulivu. Kusoma vitabu vya motisha ama msukumo huboresha hali ya moyo na kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na maradhi ya akili.

Si hivyo tu, bali pia, kusoma vitabu huongeza hekima.

10. Huleta burudani isiyo na gharama
Ni kweli, vitabu vingi vizuri huuzwa bei ghali. Lakini, usisahau kuwa unaweza kupata burudani ya karibu na bure kupitia vitabu kwa kujenga mazowea ya kutembelea maktaba katika eneo lako. Maktaba hizo huwa na mkusanyiko wa vitabu vya kila kabila, kuanzia riwaya hadi taaluma mbalimbali.

Kama unaishi katika eneo lisilo na maktaba, bado unaweza kupakua vitabu vya mtandaoni kwa kupitia rununu ama tarakilishi yako.

Hizo ndizo faida 10 zitokanazo na kupenda kusoma vitabu kama zilivoandikwa na mwandishi Lana Winter-Hébert. Kwa kuwa tunafundishwa kujali wengine, nikaonelea si vibaya nikiwashirikisha faida hizi.

Swali linaloweza kukujia kichwani, unawezaje kusoma kitabu kila siku?

Siku chache zilizopita, niliandika hapa, nikielezea niliwezaje kusoma vitabu vingi kwa mwaka 2017. Unaweza kusoma bandiko hilo, na kuona ni namna gani unaweza kutenga muda kwenye ratiba yako ngumu ya siku; hata ukapata muda wa kusoma kitabu.

Tunao msemo wa kale, maarifa hufichwa vitabuni.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Alhamisi, Januari 4, 2018.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Trending Articles