Quantcast
Channel: Fadhy Mtanga
Viewing all 76 articles
Browse latest View live

Leo ni Siku ya Mashoto Duniani

$
0
0
LEO Agosti 13, ni siku ya Mashoto Duniani (International Lefthanders Day). Siku hii imekuwa ikisherehekewa kila mwaka toka Agosti 13, 1976 pale chama cha Mashoto (Lefthanders International) kilipoitangaza siku hii kuwa maalumu kuwathamini mashoto ambao wanatengeneza asilimia 10 hadi 15 ya idadi ya watu ulimwenguni huku idadi ya wanaume mashoto ikielezwa kuwa mara mbili ya idadi ya wanawake mashoto. Madhumuni ya siku hii ni kuwakutanisha mashoto sehemu mbalimbali duniani na kufurahia upekee wao. Lakini pia siku hii inalengwa kuifahamisha dunia juu ya ukweli kuhusu mashoto.

Kabla sijaendelea na makala haya, naomba kukiri (declaring interest) kuwa mimi ni mashoto pia. Ninajivunia kuwa mashoto. Lakini pamoja na kuwa kwangu mashoto, haya ninayoyaandika katika makala haya siyaandiki kwa ufahamu wangu, bali kutokana na maandiko kadha wa kadha ambayo nimeyasoma na kuyakusanya kutoka vyanzo mbalimbali.

Mila potofu kuhusu mashoto
Kwa miaka mingi, jamii nyingi zimekuwa na mila potofu kuhusiana na mashoto. Wengi wamekuwa wakiita mkono wa kushoto kama mkono wa shetani. Jamii nyingi zimekuwa na kawaida ya kulazimisha kuwabadili watoto wao mkono wa kutumia pindi wagunduapo watoto hao ni mashoto. Jamii hizo zimekuwa zikiamini kuwa mashoto ni ulemavu ama mkosi.

Majina mengi mabaya yamekuwa yakitumiwa kwa miaka mingi yakionesha kuwadharau mashoto. Kwa mfano, hapa Tanzania mkono huo umekuwa ukiitwa ‘kono la mavi’. Katika Kilatini, mkono wa kushoto umekuwa ukitwa ‘sinitra’ ambayo humaanisha kitu kiovu.

Kumekuwa na imani kuwa mashoto wengi hukumbwa na vifo vya ajali. Lakini watafiti wamesema kuhusu hilo. Wanakiri kuwa mashoto wengi hukumbwa na ajali kutokana na ukweli vitu vyote vimetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya mkono wa kulia. Mathalani, vyombo vya moto na vyombo vingine vya matumizi ya kila siku vinawapa upendeleo wanaotumia mkono wa kulia. Kwa maana hiyo mashoto hulazimika kufoji matumizi.

Jamii zingine kwa miaka mingi zimekuwa zikiamini kuwa mashoto hukumbwa na vifo vya ajabu ajabu.

Mtazamo chanya kuhusu mashoto
Huko Peru, Amerika ya Kusini, kwenye jamii ya Inca, mashoto wanaaminiwa kuwa na uwezo mkubwa sana kiroho na uponyaji. Mtawala wa tatu wa jamii hiyo aliyekuwa mashoto alipewa jina la Lloque Yupanqui likiwa na maana ‘Mashoto aliyebarikiwa’.

Katika Ubudha, mashoto huhesabiwa ni wenye hekima zaidi.

Huko Urusi, mashoto ambao huitwa ‘Levsha’ huhesabiwa kuwa ni mafundi stadi zaidi wa kazi za mikono.

Uchina na Ujapani, mashoto huhesabiwa kuwa ni wabunifu na wachapa kazi zaidi.

Ukweli kuhusu mashoto
Sababu za msingi hasa kwa nini watu huzaliwa mashoto hazijawa wazi hadi sasa. Lakini watafiti wengi wanasema mashoto hutokana na vinasaba (genetics) na sababu za kimazingira. Inaelezwa kuwa wazazi wote wawili wakiwa mashoto, upo uwezekano wa asilimia 50 kuzaa mashoto, wakati wazazi wote wawili kama si mashoto, wana uwezekano wa asilimia 2 kuzaa mashoto.

Mashoto, kwa mujibu wa utafiti, huongozwa zaidi na upande wa kulia wa ubongo, wakati wanaotumia kulia huongozwa zaidi na upande wa kushoto wa ubongo. Kwa kuwa mashoto huongozwa na upande wa kulia, watafiti wanasema mashoto ni watu wenye uwezo mkubwa zaidi kiakili. Pia wana uwezo mkubwa zaidi katika sanaa, muziki na ubunifu kwa ujumla. Mashoto wanaelezwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa utambuzi (perception). Watafiti wanaeleza pia kuwa mashoto wana mhemuko, mchomo wa moyo ama hisia (emotions) kwa kiasi kikubwa zaidi. Hivyo mashoto wanaelezwa ni watu wenye upendo na huruma kwa kiwango cha hali ya juu sana.

Kwa mujibu wa utafiti wa Dr. Alan Searleman wa Chuo Kikuu cha Mt. Lawrence huko New York, Marekani, mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa utatuzi (problem-solving skills).

Mashoto wana uwezo mkubwa sana wa kutunza kumbukumbu kiasi kwamba wengi wao hawatumii shajara (diary) na hawapendi kutumia notebooks wanapomsikiliza mtu akitoa mhadhara.

Mashoto wana mzio (allergies) zaidi.

Mashoto wana tatizo la kukosa usingizi (insomnia) zaidi.

Mashoto huchelewa kupevuka ama kubalehe kwa miezi 4 hadi 5 ukilinganisha na wanaotumia kulia.

Mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kufikiria na kutambua mambo hususani katika teknolojia ya 3D. Wanao upeo mkubwa sana.

Mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kufanya mambo mengi sana (multi tasking). Utafiti wa Dr. Nick Cherbuin wa Chuo Kikuu cha London unaonesha kuwa mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na ndiyo sababu ni wazuri zaidi hata kwenye video games.

Mashoto wana vipaji vingi zaidi. Mashoto mmoja anaweza kuwa mchoraji, mshairi, mcheza mpira, mchonga vinyago, mwandishi wa hadithi, mbunifu wa mitindo, mbunifu wa bustani, mcheza filamu, mpigapicha, mpambaji, mwanamuziki na vingine vingi.

Wastani wa umri wa kuishi wa mashoto ni miaka 9 pungufu ya wastani wa wanaotumia mkono wa kulia.

Mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kuona chini ya maji.

Mashoto waliopo vyuoni hufanikiwa kwa asilimia 15 zaidi ya wanaotumia kulia. Na baada ya kumaliza vyuo, mashoto huwa na mafanikio kwa asilimia 26 zaidi ya wengine. Mtafiti Chris McManus katika kitabu chake cha ‘Right Hand, Left Hand’ amesema kuwa mashoto wameonesha kuwa ni watu wenye mafanikio kwa kiwango kikubwa zaidi.

Mashoto wengi baada ya masomo hufanya kazi za ubunifu zaidi kama uandishi, ushairi, muziki, uigizaji na sanaa yote kwa ujumla. Hata wanaofanya kazi zingine, huwa ni wenye kupenda ubunifu zaidi katika kufanikisha kazi zao.

Katika wabunifu watano wa kwanza wa kompyuta za Mcintosh, wanne kati yao walikuwa mashoto.

Mashoto ni wachoraji wazuri zaidi, lakini huchora michoro mingi ikiwa imeelekea upande wa kulia.

Katika marais wanne wa hivi karibuni wa Marekani, marais watatu ni mashoto. Tazama, George Bush mkubwa (mashoto), Bill Clinton (mashoto), George Bush mdogo (kulia) na Barack Obama (mashoto). Na, katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 1992, wagombea wote watatu wakubwa walikuwa mashoto. Uchaguzi wa Marekani wa 2008, wagombea wote wawili Obama na McCain ni mashoto.

Katika keyboards za QWERTY, mkono wa kushoto peke yake huweza kuchapa maneno 3400 ya Kingereza wakati mkono wa kulia peke yake huweza kuchapa maneno 450 tu ya Kingereza. Mfano wa maneno marefu ya Kingereza ambayo huchapwa na mkono wa kushoto peke yake katika kibodi ya QWERTY ni; desegregates, reverberated, watercress, aftereffects, na pia sweaterdresses.

Mashoto wana miandiko (handwriting) mizuri na yenye kuvutia mno. Na wanao uwezo mkubwa wa kuandika maandishi (herufi na tarakimu) kwa kinyume (toka kulia kwenda kushoto)

Mashoto wanapenda zaidi wanyama. Jambo la kusisimua ni kuwa dubu (bear) wote ni mashoto. Mashoto wa kiume huwapenda sana paka, na jambo la kushangaza zaidi paka wote wa kiume ni mashoto. (Naomba kukiri kuwa hili jambo linanihusu).

Asilimia 50 ya mashoto hutumia mouse za kompyuta kwa mkono wa kulia, asilimia 68 hushika mkasi kwa mkono wa kulia, na asilimia 74 hushika kitu cha chakula kwa mkono wa kulia na uma kwa mkono wa kushoto.

Watafiti wa Kikanada wanasema mashoto wanamudu kwa kiasi kikubwa zaidi kuyazowea mazingira yoyote yale. Ingawa vitu vingi vya utumizi kama milango, magitaa, visu, mikasi, magari na kadhalika vimewapendelea wanaotumia mkono wa kulia, ni mashoto ndio wanaovimudu zaidi.

Mashoto wanajiamini zaidi na ni majasiri zaidi.

Baadhi ya watu mashuhuri ambao ni mashoto
Marais wa Marekani: James A. Garfield, Herbet Hoover, Harry S. Truman, Gelard Ford, Ronald Reagan, George H. W. Bush, Bill Clinton na Barack Obama.

Watu maarufu katika historia: Joan of Arc, Napoleon Bonaparte, Julius Caesar, Michelangelo, Leonardo da Vinci, Raphael na Hellen Keller, Alexander The Great, Malkia Victoria, Mfalme George II, Mfalme George VI, Prince Charles, Prince William, Henry Ford, Benjamin Franklin, Steven Forbes na Oprah Winfrey.

Wanasiasa maarufu: Benard Membe, Fidel Castro, Ross Perot, Bob Dole, John McCain, Robert S. McNamara, Benjamin Netanyahu, Ehud Olmert na Brig. Jen. Lee Hsien Loon.

Wanamuziki maarufu: Phil Collins, Paul McCartney, Ringo Starr, Jimi Hendrix na George Michael.

Waandishi na washairi:
James Baldwin, Bet Bowen, Samuel C. Warner, Viktoria Stefanov, Diane Paul na Richard Condon.

Wacheza filamu: Charlie Chaplin, Tom Cruise, Robert de Niro, Whoopie Goldberg, Bruce Willis, Kadeem Hadson, Angelina Jolie, Marilyn Monroe, Nicole Kidman, Cary Grant, Julia Roberts,

Wacheza soka maarufu: Pele, Diego Armando Maradona, Romario na Hugo Sanchez.

Hayo ndiyo niliyoweza kukusanya kuhusu mashoto kutoka katika machapisho mbalimbali.

Natuma salamu zangu za upendo kwa mashoto wote ulimwenguni.

Heri ya siku ya mashoto duniani.


Umeme wa kulenga kwa manati

$
0
0

“UMEME na maji Tanzania ishakuwa kero…watu kero kero!”

Nimejaribu kupitia maktaba yangu kuitafuta hiyo albamu ya Wagosi wa Kaya, kundi la muziki wa Bongo Fleva liliondokea kutamba sana mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili.  Nia yangu haswa ni kuusikiliza wimbo huo.  Ingawa kundi hili liliandika wimbo huu kutokana na hali halisi pengine iliyokuwepo kwa wakati huo, naamini waliitabiria Tanzania miaka kadhaa baadaye ingekuwaje!

Ni kero hasa.  Ni kero jamani.  Ni kero kupindukia.

Unarudi nyumbani saa kumi na mbili jioni, hakuna umeme.  Na wengi wetu tunategemea umeme kuweza kupata maji ya visima.  Kwa mantiki hiyo unalala kukiwa hakuna umeme wala maji.

Unaamua kuamka saa tisa usiku wa manane walau uweze kupandisha maji ukoge kwa kuwa usiku uliopita umelazimika kulala na jasho vivyo hivyo kutokana na uhaba wa maji unaosababishwa na ukosefu wa nishati ya umeme.

Pamoja na kuamka kwako usiku huo mnene, bado hakuna umeme.

Jamani!  Simu hazina chaji.  Unakosa mawasiliano ambayo ni hitaji la muhimu sana katika ulimwengu huu tulio nao.

Unalazimika kwenda kwenye shughuli zako za kila siku, iwe kazini, kwenye biashara, shuleni, safarini na kwingineko kukuwekapo bize ukiwa na nguo zisizopigwa pasi kwa kuwa hakuna umeme.

Jamani!  Hadi lini maisha haya?

Ona sasa hata kublog sasa hivi hatuwezi tena kwani mie nina siku ya pili sasa siijui rangi ya umeme.  Na hata nilipouona ulikaa kwa dakika chache sana ambazo zisingenitosha hata kupiga pasi nusu ya shati langu la mikono mifupi.

Jamani!  Mbona kazi kweli kweli.

Kazi si kidogo!  Kweli kama ni joto ya jiwe, sasa twaiona!

Eniwei, nisiseme sana!

Nimerejea

$
0
0

fadhili 192

ASALAAM aleykum wadau.

Ni kitambo kweli sijaonekana jamvini humu.  Niliwamiss ile mbaya.  Najua nimepitwa na mambo chungumbovu.  Ilikuwa nje ya uwezo wangu.  Lakini kwa uweza wake yeye aliye juu, naamini sasa nimerejea.

Pamoja sana!

Kuanguka kwa Ghaddaf kunatoa fundisho gani kwa viongozi Afrika?

$
0
0

NILIPOANDIKA makala kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kaka yangu na mwanazuoni ninayemheshimu Profesa Matondo Nzunzullima alitoa maoni akisema, “historia haidanganyi”.  Katika makala hayo niliyoyaita, ‘Wakati ukifika umefika tu’ nilijaribu kuandika baadhi ya mambo ya kihistoria ambayo watu walikuwa wakidhania yasingewezekana.  Pengine yale makala ningekuwa ninayaandika leo, ningekuwa na jambo jingine la kuongezea.

Leo hii, dunia imeshuhudia tukio ambalo watu wengi, kwa miaka mingi sana waliamini lisingewezekana.  Nayaazima tena maneno ya Profesa Matondo, ‘historia haidanganyi’.  Dunia, leo haijashuhudia kuanguka kwa Kanali Muamar Ghaddaf tu, bali imeshuhudia ukomo wa maisha yake hapa ulimwenguni.  Ama kwa hakika, sasa Kanali Ghaddaf, kiongozi wa zamani wa Libya amemaliza vita.  Mwanafalsafa wa kale wa Ugiriki, Plato, alipata kusema, “Ni wafu pekee waliouona mwisho wa vita”.

Zamani kidogo, nilipata kukisoma kitabu kimoja cha Msumbiji, chaitwa ‘People’s Power’ kikielezea harakati za mapambano ya uhuru wa Afrika ya Kireno, Msumbiji na Angola.  Katika kitabu hicho, mwandishi (kwa bahati mbaya jina limenitoka) alielezea historia ya ukombozi wa Afrika.  Harakati ambazo waandishi Leopold Sedar Senghor wa Senegali na mshairi Aime Cesaire walipenda kuziita Negritude.  Mwandishi wa People’s Power aliandika kuwa, upepo wa ukombozi ulipoanza kuvuma katika bara la Afrika kufuatia kumalizika kwa vita kuu ya dunia, uliendelea kuvuma kwa kasi hadi ukayafikia hata maeneo ambayo hayakutarajiwa.  Hatimaye sehemu kubwa ya Afrika ikawa huru.  Mwandishi alitanabaisha kuwa, hakuna aliyeweza kuuepuka upepo huo. 

Mwishoni mwa mwaka jana wakati upepo wa mabadiliko ukianza kuvuma kwa kasi nchini Tunisia, ni wachache sana waliotarajia pengine upepo huo ungeleta athari zinazoonekana leo,  Watu wengi hapa barani Afrika, hususani viongozi wetu waliudharau sana wakidhani ni kimbunga tu cha kiangazi kinachopita kwa kasi na hatimaye hali kurejea vema.

Hata upepo huu ulivyohamia Misri na Aljeria kwa mbali, kungali watu lukuki walioona ni mambo ya Kusadikika pengine kuliko falsafa za gwiji wa falsafa katika Kiswahili, Shaaban Robert.  Kama kawaida viongozi wengi, ama niseme wote katika Afrika waliyadharau mambo yale.  Kanali Muamar Ghaddaf, alikuwa mmoja wa walioamini mambo hayo kamwe hayawezekaniki kamwe katika ardhi ya nchi aliyoiongoza kwa miaka 42.

“Historia haidanganyi”, kadri ya maneno ya mwalimu wangu Prof Matondo.  Hatimaye vuguvugu likawasili rasmi katika ardhi ya Libya.  Ghaddaf, akadiriki kuwaita wananchi wake ‘mbwa’ huku akiwaua mamia ya waandamanaji hao waliouingiza upepo wa mabadiliko nchini mwake.  Upepo wa mabadiliko ambayo kamwe hakuwahi kuyaota sembuse kuyawazia.  Huo ndio mfano haswa wa viongozi wa Afrika, kudhani wao ni miungu mtu kana kwamba hapana kiumbe ama jambo liwalo lolote chini ya jua lenye uwezo sembuse uthubutu wa kuwaondoa.

Yakawa masaa, siku, wiki, miezi ya kipute na mchakamchaka hasa wa risasi na makombora.  Hatimaye, utawala wa Kanali Ghaddaf ukaanguka rasmi.

Kanali Muamar Ghaddaf amekwishakwenda.  Kwanini tungali tukimzungumzia yeye?

Kuna somo kubwa sana kaliacha katika huu ulimwengu, hususani barani Afrika na kwingineko kwenye watawala wawaonao wananchi wao ‘vijibwa’.

Wakati ukifika umefika tu, ndilo somo kuu ambalo kila mmoja wetu angepaswa kujifunza.  Alidondoka Idd Amin Dada, Mobutu Sese Seko na wengine wengi wa sampuli hiyo katika bara la Afrika.

Viongozi wa Kiafrika wanapaswa kujitafakari upya.  Viongozi wenye tabia ya kuwadharau wananchi wao, wanapaswa kujifunza kuwa, kama alivyopata kusema mwanafasihi Ebrahim Hussein ‘wakati ukuta’ nao wafahamu hivyo.  Mwanamapinduzi na mwanareggae Bob Marley aliwahi kuimba kuwa ‘hakuna awezaye kuusimamisha muda’.  Hakuna awezaye kuuzuia muda pale wananchi wanapochoka na kuamua mabadiliko kwa gharama yoyote ile.

Wananchi ndiyo wenye nchi, kwa maana bila uwepo wao hapana haja ya uwepo wa kiongozi.  Kiongozi, kamwe haongozi majengo, wala mashamba, wala bahari, wala milima, wala mito na mabonde yake.  Kiongozi anawaongoza watu wenye utashi wa kujua mema na mabaya.  Ni watu wenye ukomo wa uvumilivu.  Ni watu wenye uwezo na uthubutu wa kufanya maamuzi. 

Viongozi wanapokuwa madarakani na kufanya mambo hovyo hovyo kwa kuwa wanawaongoza wananchi wenye hulka ya upole na mshikamano, wanapaswa kujifunza kutokana na kuanguka kwa Kanali Ghaddaf, kuwa kila jambo, liwe jema ama baya lina mwisho wake.  Tofauti ni moja, wakati jambo jema huwa na mwisho mzuri, jambo baya huwa kinyume chake.  Viongozi wasijitengenezee mwisho mbaya.

Mikataba mibovu, ufisadi na kuwadharau wananchi, ni matatizo sugu sana katika Afrika ya leo.  Wananchi wanapopiga kelele wanadhihakiwa na wakati mwingine kudhalilishwa.  Wananchi hawa wavumilivu sana.  Mwandishi Maggid Mjengwa, hapo kitambo kidogo akiandikia jarida la Rai la wakati huo, aliwahi kuandika, “hata Ivory Coast kulikuwa na amani kama Tanzania”.  Nimekuwa nikijiuliza mara nyingi maana ya maneno yale.  Yanabeba tafsiri nzito sana yenye kuhitaji tafakuri yenye umakinifu

Fundisho ambalo viongozi wetu ingewafaa kujifunza, ni kuwa hata yale mambo wanayodhani kuwa hayawezekaniki, yanawezekana sana, muda haujafika tu.  Wakati ukifika umefika tu!

Alamsiki.

Fadhy Mtanga,

Mbeya.

20 Oktoba 2011.

Airpoint

$
0
0

CAM_0183  Hapa ni Airpoint, mahali ambapo barabara ipo juu kuliko barabara zote nchini.  Eneo hili lipo barabara ya Chunya nje ya jiji la Mbeya.

CAM_0184

Hapa upo juu kabisa Airpoint.  Unalitazama Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.  Ukiwa hapo unaliona Bonde la Usangu kwa raha zako.    Utayaona maeneo kama Inyala, Chimala, Igurusi, Itamba, Msesule na kadhalika.  Utafurahia sana kuiona reli ya Uhuru inavyolizunguka eneo hilo.

Moja ya mambo niliyoyafurahia pahala hapo ni hali ya hewa yenye kusisimua mno.

Kasumulu border

$
0
0

CAM_0195

Kuelekea mpaka wa Tanzania na Malawi.

Malaria inakubalika

$
0
0

  WAKATI rais wetu alifunga safari hadi Marekani mara nyingi tu kuomba msaada wa vyandarua ili kuhakikisha malaria haikubaliki tena, hali ni tofauti katika kijiji cha Liulilo, pembezoni mwa Ziwa Nyasa huko wilayani Kyela.  Kama ambavyo tutaona katika picha zifuatazo, wakazi wa kijiji hicho ambao shughuli yao kubwa ya kiuchumi ni uvuvi, kwao malaria inakubalika kwa kwenda mbele kwa kuwa vyandarua hivyo vya msaada vina kazi kubwa sana kiuchumi badala ya kutumika kuwadhibiti mbu ambao hueneza ugonjwa wa malaria.

CAM_0307

Hapa, vyandarua vinatumika kama jamvi la kuanikia dagaa pindi wakishavuliwa ili wakauke tayari kwa kupelekwa sokoni.

CAM_0293

Hapa napo, dagaa wakikaushwa juu ya vyandarua ambavyo endapo vingeelekezwa katika matumizi sahihi kadri ya kusudio la waliovitoa, pengine ugonjwa wa malaria ungeingia katika vitabu vya historia.

CAM_0308

Hapa, vyandarua hivyo ambavyo vimeshonwa na kuunganishwa ili kuwa wavu mkubwa sana, hutumika kuvulia samaki hususani samaki wadogo wadogo kama dagaa ambao nyavu kubwa za uvuvi huwa hazifai kwa vile ni rahisi kwa samaki hao kupenya.  Picha hii inaonesha vyandarua hivyo, ambavyo sasa vimegeuka kuwa nyavu, vikiwa vimetandazwa pembezoni mwa ziwa tayari kwa ratiba ya uvuvi.

CAM_0310

Hii picha inaeleza mambo mawili.  Kwanza, nyuma kabisa vinaonekana vyandarua hivyo vikiwa vimetandazwa ardhini tayari kwa kuanikia samaki, hususani dagaa pindi waletwapo kutoka kwenye mitumbwi ya uvuvi.  Pili, mbele kabisa, vinaonekana vyandarua vikiwa vimetumika kama uzio kwenye bustani za mboga mboga ili kuwadhibiti kuku wasiharibu mboga hizo.

MAONI YANGU:  Kampeni dhidi ya malaria haitofanikiwa kamwe, endapo serikali haitokuwa makini na namna vyandarua hivi vinavyotumika.  Ukiwahoji wakazi wa eneo hilo, wanajitetea kwamba wameamua kubadilisha matumizi ya vyandarua hivyo kwa kuwa ni vidogo na havienei kwenye vitanda vyao.  Wanazidi kusema, kwa kuwa haviwasaidii, wameonelea ni vema wakabadilisha matumizi ya vyandaura hivyo. 

Kwa mtazamo wangu, huo ni utetezi dhaifu.  Lakini hata kama ni kweli, wameyafikisha wapi malalamiko hayo?  Mie nadhani bado wananchi wengi pengine hawajaona umuhimu wa kutumia vyandarua kama njia muhimu zaidi ya kuepukana na ugonjwa wa malaria.

Serikali isiishie tu kugawa vyandarua kama peremende.  Serikali inapaswa kujikita pia kwenye utafiti ili kujiridhisha endapo malengo yake yanafikiwa kwa kiwango cha kuridhisha.  Vinginevyo, serikali itakuwa inazidi kutwanga maji kwenye kinu na malaria itaendelea kutokomeza watu.

Ni hayo tu kwa leo!

Zawadi ya dagaa kwa Yasinta na Markus

$
0
0

CAM_0313

Hao dagaa wa Ziwa Nyasa ni zawadi kwa watani zangu Yasinta Ngonyani na Markus Mpangala ambao ni wapenzi wakubwa wa ugali kwa dagaa.  Ila nitajitahidi kuwatafutia walau lita mbili tatu za ulanzi kutoka Ilembula ili muweze kushushia mlo huo.


Porojo la leo: Wenyewe si mnataka kusaidiwa

$
0
0

TARATIBU Mwananchi mimi nairekebisha tai yangu.  Kisha nikaingia zangu mgahawani.  Jua linawaka vibaya mno utafikiri limeunganishwa gridi ya taifa.  Haaa!  Nilishasau humu Jamhuri ya Giza hakuna tena yale makali ya gridi ya taifa.  Siku hizi mwendo ni mgao tu miaka nenda miaka rudi na bado waziri mhusika anazidi tu kula viyoyozi kuanzia ofisini hadi kwenye gari.  Tutafanyaje sasa.

Nimeingia  zangu mgahawani hapo walau nipoze koo kwa soda baridi.  Lakini hofu yangu ni kama hizo soda baridi ntazipata maana kwa huu mgao usio na sura wala miguu wala nyuma wala mbele wala mbeleko, siku hizi soda za baridi ni anasa tupu!

“Mwananchi weweeeeee!”  Mara nasikia sauti inaniita kwa vurugu kweli.  Nageuka kumtazama anayeniita utadhani ananidai.  Heee!  Kumbe ni yule yule jamaa angu wa miaka nenda miaka rudi toka tunaendesha magari ya udongo hadi sasa tumekuwa watu wazima tunajua na stress za utawala mbovu.

“Mbona unapotea hivyo mwananchi wewe?”  Uzuri wa jamaangu huyu ni kuwa akishaanza kuongea walahi vile hakupi nafasi ya kujibu maana yeye huwa anaunganisha maswali utadhani una mashine ya kujibia.

Wakati nataka kumjibu, akazidi kubwabwaja, “Mwananchi wewe punguza kuadimika ndugu yangu….unapotea utadhani umesingiziwa kuzaliwa!”

Nikaangua kicheko.  Kisha nikairekebisha tai yangu.  “Mwananchi wewe tai yako baabkubwa sana ulinunua kwa wamachinga wa wapi?  Najua ni kwa wamachinga tu maana wewe kwa ubahili wako hauna jeuri ya kwenda kununua dukani.”

Watu wengine nao!  Isingekuwa ni rafiki yangu wa toka nitoke nakwambia Aki ya Ngai vile ningemporomoshea mvua ya matusi…maana watu tuna mastress yetu still yeye analeta makuzi.

“Tusalimiane kwanza maana unaongea tu.”  Nikaona nimtolee uvivu.

“Kwenda zako wewe!  Kwanza hebu ninunulie soda mwananchi wewe!”  Nikaona ishakuwa taabu tupu.  Kumbe mbwembwe na makelele yote hayo utadhani stendi ya Ubungo ni kutaka ofa ya soda tu hana lolote.

Nikaamua leo nami nimtolee uvivu, “We bwana wewe!  Kila siku tukikutana lazima uniombe ofa mbona wewe huwa hunipi ofa hata siku moja?”

Akaurekebisha vizuri mkanda wa suruali yake.  Alipokuwa na hakika namsikiliza, wacha aubwabwaje.  “Kwenda zako wewe…unaona ubahili kunipa ofa ya soda unanisimanga weee!  Unakuwa kama Waingereza bwana!”

Heee!  Kulikoni tena, Waingereza wamekujaje hapa?  Ikanibidi kumwuliza, “Waingereza wamekujaje hapa?”

Jamaangu akaamua kufunguka huku mate ya hasira yakimtoka mdomoni, “Nyie Watizedi hovyo kabisa.  Mmezowea kuomba omba mno misaada kwa wazungu.  Sasa kudadadeki safari hii wamewaweza!”

Nikauliza maana sipendi mafumbo mie, “Wametuwezaje?”

“Kalaghabaho!  Kumbe hujui Pinda wao Uingereza kasema msiporuhusu ushoga hampewi tena misaada!”

Kichefuchefu kikanivagaa ghafla…ama pengine nimesikia vibaya.  Nikahoji, “Unasema turuhusu wale wanaume wanaoruhusu kupumuliwa migongoni ili tuendelee kusaidiwa na wazungu?”

Jamaangu akanitizama kwa bezo.  Halafu akaongea, “We unaishi dunia ya wapi wewe?  Habari ndo hiyo.  Wazungu wamemind sasa wanasema ole wenu muwazuwie hampewi tena misaada.”

Nikamwuliza, “Hivi ndugu yangu kwani ni lazima tuishi kwa misaada?”

Kwa hasira akanijibu, “Usiwe pwimpwi wewe!  Nchi ya ajabu sana hii.  Madhahabu chungumbovu hadi wanayajengea maukuta kama ya Berlin.  Magesi usihesabu.  Maliasili ndo usiseme.  Bahari ipo. Mito ipo.  Kila kitu kipo lakini wanachakachua kila kitu wanaifanya nchi yetu iwe ombaomba kila siku.  Ndo maana tunanyanyaswa kwa sababu tumezidi mno kuwa ombaomba.”

Nikatulia najaribu kuyatafakari maneno ya rafiki yangu huyu wa miaka na miaka.  Hamu ya kunywa soda wala sina tena.  Hivi jamani jamani jamani kwanini lakini?  Kwanini tunakuwa ombaomba hadi tunawekewa masharti ya kipuuzi kabisa.

Jamaa utadhani alikuwa anayasoma mawazo yangu.  Akaanza kuongea, “Mwananchi wewe wala usisikitike sana.  Huna haja ya kuwaza sana maana haya mambo mmeyataka wenyewe wewe na marafiki zako.  Ndo matatizo ya kuchagua kwa kudanganywa na kofia na pilau.  Mnakuwa na viongozi hawana fokasi utadhani tutaacha kuwa omba omba?”

Sikumjibu kitu.  Jamaa akaendelea, “Najua huna jibu.  Wametushinda hata Libya, wamepigana vita zaidi ya miezi nane lakini umeme haujawahi kukatika.  Hawajawahi kutembeza bakuli kama lenu ambalo hadi limetoboka badala ya kukinga kwa faida ya wote misaada inavuja kwa faida ya wachache wanaolitembeza bakuli lao.”

Bado sikumjibu, “Huna jibu najua.  Sasa ndo ukawaambie wananchi wenzako wanaolalamika kila siku huko fesibuku, titwa, jamii foramu na kwingineko.  Waambie wasimlalamikie Kameruni wawalalamikie wanaoendekeza kuombaomba wakati sisi tuna kila kitu.”

Kusema kweli jamaa kanitibua nyongo yangu leo.  Aisee kumbe hali ndo ipo hivyo.

Nikaona nikiendelea kumsikiliza najiongezea stress.  Nikaondoka zangu bila hata kumwambia kwa heri!

Kwa mtindo huu ajali za barabarani hazitokoma

$
0
0

NIMEJIULIZA maswali mengi sana kichwani pasipo kupata majibu.  Siku chache zilizopita nilikuwa katika safari kutoka Mbeya mjini kuelekea Kyela, wilaya inayopakana na nchi ya Malawi.  Katika safari hiyo nimejifunza mambo mengi sana na hususani utendaji wa askari wetu wa usalama barabarani.

Wakati tukiianza safari yetu, tulifika eneo la Nane Nane ambako kuna viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya John Mwakangale.  Eneo hilo pia lina check point ya askari wa usalama barabarani.  Tukasimamishwa.  Akaja askari wa kike hadi kwenye kioo cha mbele na kuanza kukagua stika zilizopo pale.  Kisha akasema stika ya Fire imekwisha muda wake tunalazimika kulipa faini.  Hatukubishana naye, tukailipa hiyo faini ili ratiba yetu ya safari isivurugwe.

Baada ya kuilipa hiyo faini tukaruhusiwa kuendelea na safari yetu.  Hakuna ukaguzi wowote uliofanyika kwenye gari tuliyokuwa tukisafiria.  Nilishangazwa sana na kitendo cha askari kukagua stika ya Fire, huku akishindwa kukagua kama hiyo Fire extinguisher tunayo ama la.

Njiani kabla ya kufika mjini Tukuyu ambako ni makao makuu ya wilaya ya Rungwe tulisimamishwa na askari wa usalama barabarani mara nne zaidi.  Kila tulipokuwa tukisimamishwa, maswali yalikuwa ni stika ya Fire na ya wiki ya nenda kwa usalama.

Mimi sina tatizo na jambo hilo kwa kuwa hizo stika ni moja ya vyanzo vya mapato kwa serikali.  Lakini swali ninalojiuliza, je kukagua stika peke yake ndiyo njia ya kuepusha ajali za barabarani ambazo kila kukicha zinayagharimu maisha ya Watanzania?

Taifa letu na hususani askari wetu wanautazama usalama barabarani kwa macho yepi?  Nisingeshangaa endapo tungesimamishwa hata kwa nusu saa nzima askari wakifanya ukaguzi kuona kama kifaa cha kuzimia moto kipo, kuona kama breki zinafanya kazi vizuri, kuona kama indiketa ni nzima, kuona kama honi inafanya kazi, kuona kama dereva ana leseni halali, kuona kama abiria tumefunga mikanda, ama kuona kama dereva anayeendesha gari hajanywa pombe.

Tunapoteza uhai wa Watanzania wengi na wengine kuwasababishia majeraha makubwa sana na pengine ulemavu, huku wengine wakiharibiwa na kupotelewa na mali zao.  Hili jambo mamlaka zinazohusika hazioni kuwa ni tatizo.  Nasema hazioni kuwa ni tatizo kwa sababu mamlaka zinachojali, kumbe ni mapato yatokanayo na uuzaji wa stika hizo.

Ngoja niulize swali, ghafla gari husika likianza kuwaka moto, ni stika ndiyo itakayouzima moto huo?

Hivi sisi Watanzania tunafikiria kwa kutumia nini?  Ubongo huu huu ambao wenzetu wanautumia pia?  Ama sisi kuna kitu kingine tunachokitumia?  Haiingii akilini kabisa, njia nzima askari wa usalama barabarani wanakagua stika kwenye magari.

Barabara zetu zimejaa magari mabovu mabovu.  Kuna gari ukiliona njiani unajiuliza mara kumi kumi, hivi hili gari linaruhusiwaje kutembea barabarani?  Wakati nikiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuja Mbeya, nilikutana na jambo la kushangaza sana njiani.  Kuna basi kutoka Iringa kwenda Dar lilikuwa linatembea upande upande kiasi cha kuyafanya magari mengi yawe yanapaki pembeni kulipisha.

Nikajawa na maswali kichwani.  Hivi hawa askari wetu ambao kodi zetu ndizo zinazowalipa mishahara wanaujua wajibu wao?  Kuliacha basi lisafiri kutoka Iringa hadi Dar katika hali kama ile, hakuhatarishi tu usalama wa abiria na mali zao ndani ya basi hilo, bali pia usalama wa watumiaji wengine wa barabara hiyo.  Ni jambo ambalo si tu linashangaza, bali pia linasikitisha na kufedhehesha.

Na basi kama hilo, pamoja na magari mengine maelfu kwa maelfu yaliyo mabovu barabarani, yanazidi tu kutembea kwa kuwa askari wetu wa usalama barabarani wanakazana na ukaguzi wa stika za fire na wiki ya nenda kwa usalama.  Wacha niseme msimamo wangu, wiki ya nenda kwa usalama sioni mantiki yake zaidi ya kutumia tu pesa kwa wananchi wakati magari mabovu yanazidi kutembea barabarani.

Siku moja nimesafiri kwenye basi dogo la abiria, Coaster kutoka Mbeya kwenda Tunduma, mji wa mpakani na Zambia.  Coaster ile honi yake haikuwa ikifanya kazi.  Lakini jambo la kushangaza ilisafiri kutoka Mbeya hadi Tunduma pasipo matatizo yoyote na askari wa usalama barabarani.  Sasa leo nijiulize swali, kati ya honi ya gari na stika ya fire, kipi kinapokosekana kina madhara makubwa kwa usalama wa raia na mali zao?

Labda nisaidiwe kuelewesha umuhimu wa hizo stika kushinda umuhimu wa vitu kama honi, kizima moto, breki, taa, mikanda, leseni na kofia kwa waendesha pikipiki.

Lakini kama stika za fire na wiki ya nenda kwa usalama ni muhimu zaidi kukaguliwa kuliko hivyo vitu vingine, basi wacha tu nimalize kwa kusema, kwa mtindo huu, ajali za barabarani hazitokoma.

Siku njema.

Fadhy Mtanga,

Mbeya.

4 Novemba 2011.

CCM na hadithi ya mwanaume aliyeyasahau majukumu yake

$
0
0

ILIPATA kutokea pahala fulani mumu humu ulimwenguni.  Paliondokea mwanamume mmoja awaye rijali.  Mwanaume huyo alisifika sana kijijini kwake kutokana na uchapakazi wake.  Mwanaume huyo alijenga nyumba nzuri kweli.  Nyumba hiyo ilipendeza kijiji kizima.  Hata vijiji vya jirani, hapakuondokea kifani chake.

Mabinti makumi kwa makumi.  Pengine mamia kwa mamia, walitamani sana kuposwa na mwanaume yule.  Walizisikia sifa zake.  Wengine walijionea sifa zake kwa macho yao.  Alikuwa na akili nyingi sana.  Minguvu nayo tele tele.  Alilima mazao kwa jitihada zake zote na kuwa mfano wa uzalishaji kijijini pale.

Si punde, mwanaume huyo akaposa mwanamke katika mmoja wa wale makumi ama mamia ya wanawake waliotamani na kumendea kuposwa naye.  Ilikuwa sherehe kubwa sana kijijini.  Wakaalikwa marafiki, jamaa na ndugu kutoka vijiji vya jirani wapate kuwa mashuhuda wa ndoa hiyo. 

Mwanamke huyo alikuwa na uzuri usioweza kufananishwa na kitu chochote.  Kila mtu akamwonea gere.  Hata wanawake wenzake wakakiri kuwa binti huyo amehitimu ulimbwende na umaridadi.  Wakasema ni stahili yake kuposwa na mwanaume huyo.  Kuna wanaume lukuki walijaribu kurusha kete zao kwa mwanamke huyo pasi na mafanikio.  Wakaishia kula kwa macho huku udenda ukishindwa kuwakatika.

Siku nazo zikasogea pasina ajizi.  Mwanaume yule akiwa na mwanamke ambaye sasa ndiye mkewe.  Mwanamke huyo alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mumewe.  Alimheshimu.  Alimsikiliza.  Alimjali na kumthamini pia.  Mwanamke huyo akawa mwaminifu sana kwa mumewe.  Ijapokuwa wanaume wengi sana bado waliendelea kujaribu kumtongonza, hawakuambulia chochote.  Mwanamke huyo aliwakatalia katakata kwa kuwa alilidhika na mumewe.  Awakubalie kwa lipi hasa wakati huduma zote anapewa na mumewe?

Si punde, mwanaume yule akabweteka.  Akaanza kiburi na bezo kwa mkewe.  Akajiona yeye ndiye yeye na hapana mwingine awaye yeyote wa kumfikia.  Akaanza kumpiga na kumwumiza kupindukia.  Akaacha kumpa huduma nzuri.  Akaanza kumnyonya hata kile kidogo alichokuwa nacho huyo mkewe.  Mwanamke wa watu akachakaa ghafla.  Hali yake ikazidi kuwa duni zaidi.

Lakini jambo la kustaajabisha zaidi, mwanaume huyo akazidi kuwa mjivuni.  Hakuacha kupayuka kuwa yeye ndiye yeye, hapana yeyote amfaaye mke wake.  Akazidi kupayuka kuwa wanaume wengine wanaommendea mkewe wanajisumbua bure kwa kuwa kamwe, asilani abadan, hawatoweza kumpata.

Wanaume wenzake wakayasikia maneno hayo.  Mkewe naye masikio yake hayakuwa likizo.  Yakalidaka kila neno.  Chambilecho wahenga, wanyimwa mlo, katu si maneno.  Wanaume hao pamwe watu wengine wakamwambia mwanamke huyo juu ya majigambo ya mumewe.

Mwanamke huyo akafikiria sana.  Kwa nini aendelee kuteseka kwa mume asiyemjali wala kumthamini ilhali kuna wanaume wengine chungu mbovu wenye nia ya kweli na mapenzi mema kwake?  Kwa nini lakini?  Bado mwanamke huyo hakupata jibu. 

Akaendelea kufikiria kwa makini.  Akapata jawabu kuwa kwa kuwa amekaa kwenye ndoa hiyo kwa muda mrefu, haikosi mumewe keshabweteka na kujisahau.  Akagundua hiyo ndiyo sababu mwanaume ambaye ni mumewe wala hana muda naye.

Akaamua kumkubali mwanaume mwingine.  Mumewe alipogundua akaja juu kweli.  Kwa nini mkewe ampe nafasi mtu mwingine?

Bila ya woga, wala kumung’unya maneno, mwanamke wake akamjibu, “Umeshindwa kutimiza wajibu wako, wacha wengine wenye uwezo waje kutimiza.”

Basi, mwanaume yule akakasirika sana.  Akaamua kumzushia mwanaume mpya maneno ya uwongo ili jamii imchukie.  Pia akamfanyia visa mbalimbali ili aonekane asiyefaa.

Akasahau kuwa wema hushinda uovu.

Fadhy Mtanga,

Mbeya, Tanzania.

19 Novemba 2011.

Riwaya ya Kizungumkuti kutoka kwa Fadhy Mtanga

$
0
0

kava kizungumkuti

Wadau,

Asalaam aleykum!

Nimekuwa kimya kwa kipindi kirefu katika ulimwengu wa kublog.  Chambilecho wahenga, kimya kingi kina mshindo mkuu.  Sikuwa kimya kwa kuwa labda nimechoka kublog.  La hasha.  Nilikuwa kimya kwa kuwa nilikuwa jikoni, nikikimbizana na moto wa kuni katika upishi.  Upishi wa pishi la riwaya ya Kiswahili.

Pishi lipo katika hatua za mwisho.  Si punde litapakuliwa.  Litawekwa mezani.  Likishawekwa mezani, ni wakati mahsusi kwako kula kadri ya uwezo wako.

Ninayofuraha kukuleteeni kitabu cha kwanza cha riwaya.  Ni riwaya ya kwanza kuichapa katika miswada mingi niliyoiandika kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Riwaya ya KIZUNGUMKUTI…..

Riwaya itakayokukutanisha na Hafsa Hashim….msichana mweledi, mstahamilivu, mwenye subira, mwenye hekima…..mwenye upendo wa kweli kwa mumewe….mwenye furaha tele ndani ya ndoa yake.  Mwanamke aliyeamini furaha hiyo itadumu daima dawamu, kabla jinamizi la mahusiano yake ya nyuma halijajitokeza na kusababisha jitimai katika ndoa yake.

Riwaya itakayokuweka jijini Dar es Salaam….kisha ikakuondoa na kukusafirisha hadi Songea, Iringa, Mbeya, Kyela, Chunya, Mkuranga, Dodoma, Zanzibar, Moshi….hadi Arusha… Kote huko katika jitihada za wahusika kukabiliana na Kizungumkuti kilichoyasibu maisha yako. 

Ni visa na mikasa vya mapenzi ya kweli….mapenzi ya uwongo…usaliti wa kikulacho kilicho nguoni mwako…matumizi mabaya ya vyombo vya umma…urafiki wa kweli….imani…ushirikina….na zaidi, hekima ya hali ya juu katika kukabiliana na misukosuko ya ndoa.

Kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, riwaya hii inatarajiwa kuwa sokoni kuanzia siku ya Jumanne, Januari 2, 2012.

Karibuni sana kwa ununuzi wa riwaya hii.

Pole kwa Watanzania wote

$
0
0

NI SIKU mbili sasa, taifa linazizima kwa habari za kushitua mioyo kuhusiana na mafuriko makubwa katika jiji la Dar es Salaam.  Hali ni mbaya zaidi.  Mvua inanyesha kwa kiwango kikubwa mno ambacho wataalamu wetu wanasema hakijawahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka hamsini.

Ndugu zetu waliopo mikoani hawana raha kabisa.  Lazima wakose raha kwa kuwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanawahusu kwa namna moja ama nyingine.  Ndugu zetu waliopo nje ya nchi hawana amani.  Wote kwa pamoja hawaishi kuulizia juu ya mustakabali wetu.  Wanapoona kwenye runinga, wanashindwa kula wala kulala wakijawa hofu tele nini hatma yetu ndugu zao tuishio katika mji huu uliokumbwa na maafa haya.

Nyumba zinazama, barabara zinabomoka, madaraja yanavunjika, mali nazo zinaharibika vibaya sana.  Eneo moja linakosa mawasiliano na eneo jingine ndani ya mji huo huo.  Wanafamilia wanapoteana katika harakati za kuyaokoa maisha yao.

Hali ni tete mno.

Kwa unyenyekevu mkubwa mno, na kwa upendo wa dhati, na kwa hisia za moyo wangu, ninapenda kutoa pole kwa Watanzania wenzangu wote.  Ninajua kila mmoja wetu ameathiriwa na kuumizwa na maafa haya yanayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini hapa.

Ninajua ni kipindi kigumu sana ambacho taifa linakipitia.  Ni kipindi kigumu sana kwa kuwa maelfu ya watu hawana makazi.  Ni kipindi kigumu kwa kuwa mali zinapotea.  Ni kipindi kigumu kwa kuwa familia zinapotezana.  Ni kipindi kigumu kwa kuwa ni vigumu hata kupata mahitaji muhimu kutokana na kuathiriwa kwa miundombinu.  Na, ni kipindi kigumu kwa kuwa tupo katika hatari ya mlipuko mkubwa sana wa magonjwa.

Dar es Salaam si salama.

Kama taifa, tunaungana katika kipindi kigumu kama hiki.  Tunaungana tukiwa tumeweka kando tofauti zetu kisiasa, rangi, kabila, dini, jinsia, na hata taifa.  Tunasimama pamoja katika kufarijiana ili tuweze kukabiliana vema na kipindi hiki kigumu mno.

Poleni sana Watanzania wenzangu.

Ingawa si busara kupeana lawama katika nyakati ngumu kama hizi, mie ninaomba kwa unyenyekevu nitoe lawama zangu leo.  Katika pitapita zangu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kumekuwa na wimbi la lawama kwa wakazi waliojenga makazi yao mabondeni.  Hawa wanaonekana wamejitakia maafa haya.

Nitakuwa mtu wa mwisho kuwalaumu wakazi hao wa mabondeni.

Lakini, sitosita kuzilaumu mamlaka.  Ninawalaumu Watanzania wenzetu tuliowapa dhamana ya kutuongoza.  Ninawalaumu hao.  Ninawaona kama chanzo cha maafa makubwa kwa wakazi wa mabondeni.  Nitawalaumu wao daima kwa maafa kama haya.

Kwa nini ninawalaumu Watanzania wenzetu tuliowapa dhamana ya kutuongoza?  Jibu ninalo.  Watanzania hawa tumewasomesha kwa kodi zetu na rasilimali zetu.  Tumewasomesha ili wawe wataalamu wa mipango miji.  Tulitaka waende shule wakajifunze namna bora ya kupanga miji yetu.  Tena wengine tukawapeleka hadi ng’ambo ili pamoja na kusoma, waone kwa wenzetu na kujifunza jinsi miji yao inavyopangwa.

Walipohitimu, tukawapa dhamana ya kuwa wapangaji wa miji yetu.  Wengine tukawapa dhamana wawe wasimamizi wa sera na sheria zetu.  Wengine tukawapa dhamana wawe wasimamizi wa pesa zetu.  Wengine tukawapa dhamana wasimamie sheria zetu zisivunjwe.  Hawa wote ni Watanzania wenzetu ambao tumekuwa na imani na usomi wao na utaalamu wao, tukitegemea uwe wenye manufaa kwa taifa zima.

Wakapewa madaraka, wakalala usingizi.

Miji haikupangwa tena.  Ramani za miji wakazifungia makabatini ziliwe na panya.  Wao wakalala usingizi wa pono.  Wananchi, kwa kuwa hawana elimu, wala uwezo wa kuridhisha kifedha, wakaanza kujijengea makazi wasitiri familia zao.  Kwa kuwa hakuna mipango ya miji, wananchi wakajenga tu.  Kwa kuwa hakuna wasimamizi wa sheria, wananchi wakajenga tu.  Kwa kuwa hakuna elimu nzuri kwa wananchi juu ya madhara ya ujenzi holela, wananchi wakajenga tu.  Wakajenga tu.  Wakajenga na kujenga na kujenga.  Wakajenga tu.

Maafa yakaanza kutokea.

Nikiwa sekondari miaka ya tisini, nikaanza kumsikia mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wa wakati huo, Luteni Mstaafu Yusufu Makamba.  Nikamsikia akiwapigia kelele waliojenga mabondeni wahame.  Baada ya hapo, kila mwaka nimekuwa nikizisikia kelele za watu wahame mabondeni.  Wahame.  Hameni.  Hameni jamani.  Kwa hiyari na kwa lazima, hameni hameni.

Toka nilipoanza kuzisikia kauli hizo, nikaanza kutawaliwa na maswali kichwani mwangu.  Kwa nini wahame mabondeni? 

Wanapoanza kuchimba msingi ili wajenge nyumba serikali haikuwaona?  Kuta za nyumba zao zilipoanza tu kusimama, serikali ilikuwa wapi?  Hawa wasomi wetu walikuwa wapi kufanya tathmini na kupanga miji yetu vizuri ili miundombinu ya maji taka ijengeke vizuri?  Hapo ndipo ninapoanza kupata mashaka na weledi wa wasomi wetu.  Kuna mtu mmoja aliwahi kusema kuwa, GPA si kipimo cha ujuzi wa mwanazuoni.  Wapo wanaopata GPA nzuri kutokana na uzuri wao katika kuiba mitihani.  Sasa naanza kuyasadiki maneno haya.

Kama tuna wasomi walioshindwa kuplani miji yetu.  Kama tuna wasomi walioshindwa kusimamia vema sheria zetu.  Kama tuna wasomi wanaoshindwa kutuongoza vema.  Nini tunaweza kukisema juu ya weledi wao?  Nini tunaweza kukisema juu ya uinjinia na udaktari na uprofesa wao?  Kwangu jibu lingekuwa jepesi tu, vyeti vyao ni vya magumashi.

Hawa sasa, kwa mtazamo wangu, ndiyo wenye kuzistahili lawama kwa ujenzi holela wa makazi.  Hawa wanaokaa maofisini kwenye viyoyozi na viti vya kuzunguka.  Hawa wanaohudhuria warsha, semina, makongamano, majukwaa, mijadala na kila kitu.  Hawa wanaolipwa mamilioni kwa mamilioni ya pesa zetu sisi tunaotaabika na maafa haya.  Hawa wanaosahau wajibu wao kwa taifa ni nini?  Hawa ndiyo wasababishi wakubwa kwa ujenzi huu holela ambao unayafanya maafa haya kuwa ya kiwango kikubwa kiasi hiki.

Laiti kila mtu angeutimiza wajibu wake itakiwavyo, leo tusingekuwa na ujenzi holela.  Leo tusingekuwa na madhara makubwa sana kutokana na mafuriko haya.  Leo tungekuwa na uokoaji wenye urahisi kabisa kuliko ilivyo sasa.  Kama tu, kila mmoja angeutimiza wajibu wake itakiwavyo.

Nimalizie tu kwa kurudia kuwapeni pole nyingi Watanzania wenzangu.  Mwenyezi Mungu akufanyieni wepesi katika kila jambo.

Mungu Ibariki Tanzania.

Fadhy Mtanga,

Kijitonyama, Dar es Salaam.

22 Disemba 2011.

Heri ya siku ya kuzaliwa mama yangu

$
0
0
Heri ya siku ya kuzaliwa mama yangu mpenzi. Leo tarehe 18 Januari ni siku muhimu sana kwangu. Ni siku ambayo mama yangu mpenzi ulikuja duniani. Ni siku iliyoandaa uwepo wangu duniani.

Mama, leo tunapoikumbuka siku hii ya thamani zaidi, napenda kukwambiia kuwa ninakupenda sana. Kwangu hakuna zaidi yako. Ninamshukuru sana Mungu kwa ajili yako. Ninamshukuru sana Mungu kwa kuwa pamoja na kunilea kwako ukiwa peke yako, umenifanya kuwa hivi nilivyo leo. Ninajivunia sana wewe.

Ninakushukuru sana mama kwani magumu yangu yamekuwa yako pia, mepesi yangu yamekuwa yako pia. Umekuwa ukiniunga mkono daima. Umekuwa ukinikosoa pale nipotokapo. Umekuwa ukinifuta machozi na kunikumbatia hata wengine wote wanipapo kisogo. Umekuwa ukinipa moyo wengine wanineneapo ubaya. Kwangu, wewe ni mwanamke wa shoka.

Mama, leo ni siku muhimu sana kwangu. Ninakuombea maisha marefu sana, yenye furaha tele, afya njema, na mafanikio zaidi. Ninakupenda sana mama yangu. Ninakupenda mno. Ninamshukuru sana Mungu kwa kunipa wewe kama mama yangu.

HAPPY BIRTHDAY MY LOVELY MOM!

Porojo la leo: Upepo hupita tu

$
0
0

“MV MAPENZI…meli ya wapendanao…moyo kama bahari manahodha mimi na wewe….kuchafuka kwa bahari siyo mwisho wa safari…meli ilipokumbwa na dhoruba nahodha akajitosa baharini….wale papa na nyangumi wenye uchu…wamemmeza ooh masikini…..”  Nimetulia zangu kwenye kakibanda kangu nikisikiliza santuri za enzi za muziki ulipokuwa muziki.  Nimetulia kweli kweli wala sina hiyana na mtu.  Muziki ni mtamu kweli kweli.  Muziki huu unanikumbusha enzi zangu zile nami nilipokuwa na jeuri ya kusimama mbele za watu nikazungumza nikasikilizwa.  Kweli wakati ni kama upepo ukienda haurudi .  Kama maji ya mto yakishatiririkia huko mabondeni, thubutu yake kurejea.

“Mwananchi weweeee!”  Mara nasikia sauti ikiita kwa nguvu kutokea nje.  Ni dhahiri mwitaji huyo anatembea kuelekea mlangoni kwangu.  Nani huyo?  Anataka nini kwangu?  Napunguza sauti ya muziki ili nisikilize vema.  Sauti inarudia kuita.  Tena awamu hii ikiashiria kuwa mgeni huyo yu tayari mlangoni akingoja tu mlango kufunguliwa.  Naitazama saa yangu niliyoachiwa na mzungu nikiwa bado kijana tu miaka hiyo ya zidumu fikra.  Saa haichoki hii.  Miaka nenda rudi watu wanazaliwa wanakuwa hadi wanakufa lakini saa hii ya Mswisi haichoki.  Saa yangu inaniambia ishatimu saa sita na robo za mchana.

Nakwenda hadi mlangoni.  Sasa nimekwishaitambua sauti.  Najiuliza maswali lukuki wakati nikiusogelea mlango ili kumfungulia mgeni huyo asiye na ajizi kuja kwenye majumba ya watu mchana mantashahu kama huu wakati wenzake tunajiandaa na mambo ya madikodiko.  Maana kwa maisha ya sasa ukiona unapata mgeni wakati wa maakuli ujuwe kuna jambo  tu…lazima mgeni huyo yupo mawindoni.

“Karibu sheikh wangu!”  Namkaribisha mgeni wangu.  Sijakutana naye siku nyingi sana ni kama miezi sita hivi.  Unamkumbuka yule rafiki yangu amabaye huongea pasi breki?  Basi ndiye huyu kaja leo.  Najua hajaja bure bure lazima ana jambo maana jamaangu anapenda kulalamika ile mbaya.  Yeye kila jambo ni kulalamika tu.

“Karibu…karibu sana maalim.”  Nazidi kumkaribisha baada ya kuona kabung’aa tu.

Namkaribisha kwa mara nyingine, “Karibu sana ustaadh wangu.”

Mara akaangua kicheko.  Tobaa!  Nini tena kimchekeshacho kwa kiasi hiki?  Ikanipasa kuhoji kulikoni, asije akawa kashikwa wehu mie nikadhani masikhara.  “Mbona wacheka al-watan?”

“Utaniita majina yote mpuuzi wewe!”  Akalifungua domole.

Nikataharuki.  “Mpuuzi mimi huyu?  Tokea lini?”

“Ndiyo mpuuzi sana.  Ndiyo nini umetutenda?  Miezi sita sasa huonekani? Simu hupatikani?  Kijiweni huji tena.  Porojo wala hatuzipati tena.  Ulisafiri?  Kusafiri gani huko huwezi hata toa neno la kwa heri?  Tabia hii umejifunzia wapi? Na lini?  Nani kakufundisha?  Mwananchi wewe hufai hata bure ndugu yangu.  We unajisikiaje kututenga hivyo wenzako masiku yaja yaenda?”

Si nilisema, huyu jamaa akishaanza kuongea hakupi nafasi ya kupumua.  Sijui huwa anafikiria saa ngapi.  Nikaona isiwe taabu.  Nikamkatisha.  “Sikufanya makusudi ndugu yangu.  Ni hadithi ndefu.  Nisamehe bure.”

“We’ kila siku hadithi ndefu tu kama The Great North Road.  Umeadimika hadi hujui yanayotokea mtaani kwetu.  Sasa kwa taarifa yako hiyo nyumba hapo wenye nyumba wamecharuka kweli.  Wanataka wapangaji wao wabwage manyanga waondoke ili wawapishe wapangaji wengine.  Mi nakwambia nyumba ya moto kweli kweli ungekuwepo ungejionea mwenyewe.  Tatizo wapangaji wana kiburi sana na kila siku wanazidi kuiharibu nyumba.  Wenye nyumba weshawachoka wapangaji wale.”  Jamaa akafunguka.

Nahisi sikuwa nimemwelewa.  Nikahoji, “Kwani tatizo ni nini hasa?”

Chapchapu kanijibu, “Tatizo ni nini?  Unataka kujua tatizo?  Wapangaji wale hawana utu.  Hawana huruma.  Wanaiharibu nyumba utadhani ya kwao wao tu.  Eti hata wale wayama kule bandani nasikia wapangaji hao wanawauza kinyemela kwa marafiki zao wa vijiji vya mbali.  Yaani patashika bin sokomoko bin songombingo.  Tena nikwambie rafiki yangu wale wapangaji ovyo kabisa.  Hata yule mwenye jukumu la kuwasha moto ndiyo hovyo kabisa kila siku watu hawana moto.”

“Sasa kwa nini dalali wao na yule mpangaji mkuu wasiwatimue ili walete wapangaji wengine?”  Nikamwuliza swahiba wangu.  Kumbe kujifungia ndani kumenifanya nikose mambo mengi sana.  Afadhali huyu jamaa leo kaja kachangamsha kichwa changu.

“Aah wapi!  Dalali alituzuga angemwambia mpangaji mkuu awatimue lakini hakuna kitu.  Mpangaji mkuu anadai huu ni upepo tu wa kimbunga.”

Nikamtupia swali.  “Kwa hiyo anaamini kama upepo lazima utapita tu na kwenda zake?”

“We wa wapi wewe mwananchi wewe?  Upepo huwa unapita siku zote.”

“Hata mimi naamini utapita tu si upepo huu!”  Nami nikaongezea.

Jamaa yangu akaja juu ghafla.  “Usiwe bwege-mtozeni mwananchi wewe.  Nawe na ujanja wako wote unakimbilia tu kusema upepo utapita tu.  Sawa hata upepo ukipita tu ukaenda zake unajua kinachotokea nyuma yake?”

“Nikamjibu haraka.  “Vumbi tu!”

“Wewe kweli hamnazo.  Vumbi?  Ingekuwa vumbi si afadhali!  Kwa taarifa yako upepo haupiti hivi hivi.  Kuna upepo huwa unaezua bati.  Unavunja miti.  Unabomoa milango na madirisha.  Na mwingine, unaacha nyuma kwenye nyumba.”

Nikadakia.  “Kwa hiyo unataka kusema?”

Hakunichelewesha.  “Upepo hata ukipita haupiti bure bure wewe!  Kama nawe unajiridhisha hivyo shaurilo.”

“Utapita tu sheikh wangu.”  Nikasisitiza.

“Kalaghabhaho!”


Najiuliza kuhusu huyu mfanyakazi

$
0
0

Mfanyakazi anayelipwa 150,000/=...kapanga chumba kimoja tu ambacho kodi ni 30,000/ kwa mwezi (bado atalazimishwa alipe kodi ya miezi 6 ama mwaka 1 wakati analipwa mshahara kwa mwezi). Anaishi Yombo Makangarawe na kufanya kazi Posta (Ameshindwa kupanga karibu kutokana na kutomudu gharama) Kila siku anatumia 1200/= kwenda na kurudi kazini. Kama atakwenda kazini kwa siku 22 tu kwa mwezi, atalazimika kutumia sh 26,400/= Kama kila siku mchana atakula 1,000/= akiwa kazini (hivi bado Posta kuna chakula cha bei hiyo?) kwa hizo siku 22 atatumia 22,000/= (hapo hata jua liwake vipi asijiroge kununua maji ya kunywa vinginevyo kaharibu bajeti)

Turudi kwenye familia anayoiacha Makangarawe ya mke na mtoto mmoja tu. Inalazimika kulipia umeme 20,000/= kwa mwezi (ambao hata hivyo unakatika muda mrefu na kumwongezea bajeti ya mafuta ya taa) Inalazimika kununua mkaa wa kupikia ambao gunia moja ni 24,000/= (hana jeuri ya kutumia gesi na umeme kupikia).

Turudi kwenye chakula cha familia nzima.  Kama watajibana mno na kula sh 2,000/= tu kwa wastani kwa siku (Sijui watakula nini maana bei ya mchele, sukari na maharage dukani haikamatiki kwa mtu kama yeye) kwa mwezi moja atalazimika kutumia jumla ya sh 60,000/= kwa chakula cha familia yake.

Kama atajibana na kuishi kwa mahesabu hayo, atalazimika kila mwezi kukopa sh 32,400/= ambazo sijui atazilipa kwa chanzo kipi cha mshahara.

Hapo nimezungumza kijuu juu kutengeneza mantiki, lakini sijazungumzia habari za kodi, makato ya mifuko ya hifadhi ya jamii, na makato mengine.  Hapo sijazungumzia gharama za matibabu, mambo ya kifamilia na kijamii kama misiba na kadhalika.  Sijazungumzia karo za shule na gharama zinazoambatana.

Sijazungumzia mengi tu yanayogharimu.  

Najiuliza swali linalozaa maswali.  Mfanyakazi kama huyu bado anahimizwa uzalendo na kuipenda serikali yake na chama cha hiyo serikali?  Mfanyakazi kama huyo likitokea 'dili' kazini atabakiwa na moyo wa uaminifu na uadilifu?

Mfanyakazi kama huyu ambaye kila siku anawaona mawaziri na watendaji wengine serikalini wanavyoishi maisha ya kifahari na kujilimbikizia mali, ambaye ana hakika kabisa endapo watendaji serikalini wangefanya kazi kwa uaminifu mkubwa basi maisha yake yasingekuwa ya dhiki kubwa hivyo.  Mfanyakazi kama huyu atakuwa na furaha na amani moyoni mwake?

Mfanyakazi kama huyu, ambaye ikitokea mmoja katika familia akaugua siku mbili tu, basi yeye anabaki na madeni, bado tunamtaka aipende serikali yake?

Najiuliza tu jamani.  Si lazima nijijibu, kwa kuwa sina uwezo wa kujijibu.

Heri ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Nawapendeni nyote.

Fadhy Mtanga,
Sinza.
Mei Mosi, 2012.

Barua kwako mpenzi wangu

$
0
0

Mpenzi wangu,

Nikupendaye kwa dhati kutoka moyoni mwangu,

Nakusalimia salamu ya huba iliyoambatana na busu motomoto.

Mpenzi wangu nianze kwa kukushukuru sana kwa barua yako iliyojaa huba ambayo nimeipokea jana mchana nikiwa kazini. Niseme tu nimefurahi sana mpenzi wangu kupata barua yako. Siku zote barua zako huwa tiba mahabuba moyoni mwangu. Kila niusomapo mwandiko wako wa kimahaba huwa napata liwazo la haja moyoni mwangu. Maneno ya kwenye barua yako ni dawa isiyo na kifani ndani ya moyo wangu. Kila mara najikuta moyo wangu unaongeza maradufu upendo juu yako.

Mpenzi wangu, usishangae kuwa nimepata barua jana lakini nimechelewa kukujibu hadi leo ndiyo nimeshika kalamu na karatasi ili nikuandikie ewe malaika wa moyo wangu. Nilipoipata barua yako nilitafakari kwa muda mrefu mno hadi kujikuta nikitokwa na machozi. Hayakuwa machozi ya furaha kama yale yanidondokayo kila wakati nisomapo maneno matamu kutoka kwako ewe mwandani wangu. Maneno ya kwenye barua yako yamenichoma moyoni mwangu mithili ya mkuki wenye ncha kali tena iliyoiva vilivyo kwenye tanuru la moto. Mpenzi wangu, niliyekuchagua mimi mwenyewe kutokana na hisia kali na mapenzi mazito sana niliyonayo moyoni mwangu juu yako, amini bado nakupenda sana.

Mpenzi wangu, nikakiri kwa yakini kuwa nilikuahidi toka miaka mingi sana kuwa pindi nitakapojaaliwa kupata kazi nitakuoa. Nayakumbuka maneno ya ahadi niliyokuwa nikikupa kila mara tulipokuwa tukipata kaupenyo ka kuwa pamoja. Ahadi yangu bado ipo pale pale mpenzi wangu. Moyo wangu, kwa dhati kabisa, bado una dhamira ya dhati ya kukuoa mpenzi wangu nikupendaye kuliko chochote humu duniani, kuliko hata niipendavyo nafsi yangu. Bila wewe mpenzi wangu, dunia hii ina faida gani kwangu?

Mpenzi, nimetokwa machozi kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe. Kwenye barua yako umeandika jinsi unavyokata tamaa kwani sasa ni mwaka moja toka nianze kazi lakini sijatimiza ahadi yangu ya kukuoa. Mpenzi unaona kama nakupotezea muda na unaniomba kama sina haja nawe nikupe nafasi uolewe na mtu mwingine ambaye hata leo hii yupo tayari kuleta posa kwa wazazi wako. Sijui niyaelezeaje maumivu makali ninayoyasikia ndani ya moyo wangu.

Mpenzi wangu, niseme tu ukweli. Ninakupenda mno kuliko hata maana ya neno lenyewe upendo. Ninatamani sana hata sekunde hii hii niwe nimeoana nawe. Lakini, kama nikwambiavyo siku zote, ugumu wa maisha hapa Dar es Salaam hususani kwangu mie mfanyakazi wa kima cha chini ndiyo unaonifanya nikose uthubutu wa kukuoa ewe mpenzi wangu niliyekupa moyo wangu wote, haraka iwezekanavyo kama ambavyo nimekuwa nikikuahidi mara nyingi sana. Mpenzi wangu, moyoni mwangu inaniuma sana maana maisha magumu ninayoyaishi hapa Dar es Salaam kwa kweli yanatishia kwa kiasi kikubwa sana ustawi na uhai wa penzi letu.

Mpenzi wangu, nikwambie nini ili ufahamu kwa kiasi gani akili na moyo wangu vyatamani kwa dhati kabisa kuishi nawe milele yote kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujaalia siku za kuishi humu duniani. Nikwambieje ili ufahamu ni namna gani nalitamani pendo hili lidumu humu duniani na baada ya hapo?

Mpenzi, maisha yangu mfanyakazi wa kima cha chini ni magumu mno. Fikiria mpenzi wangu, kamshahara kangu ambako ni kadogo mno, kanapaswa kalipe kodi ya nyumba, umeme, maji, matibabu, gharama za usafiri na mengineyo chungumbovu. Mpenzi wangu huwezi amini kuna wakati huwa nalazimika kutembea kwa miguu kutoka kazini pale Stesheni mjini hadi nilikopanga Mbagala Kizuiani. Huwa inanigharimu masaa karibia mawili nachapa tu mwendo tena wakati mwingine mvua ikininyeeshea mwili mzima. Sijakwambia tu mpenzi wangu, mara zingine huwa nalazimika kushindia mlo mmoja ama pengine nisile kabisa. We acha tu mpenzi wangu.

Mpenzi, natamani ningekuwa na uwezo wa kukufungulia moyo wangu uyaone yaliyo ndani. Natamani mno tena kupita maelezo kuoana nawe. Kinachonikwamisha mpenzi wangu ni ugumu tu wa maisha ninaokabiliana nao hapa mjini. Sikusudii kukuoa ili uteseke. Sikusudii kukuoa ili nikushindishe njaa. Siyakusudii hayo.

Mpenzi wangu, sikusudii kuuweka uhusiano wetu rehani. Mpenzi sina namna niwezayo kuibadili hali halisi kwa sasa zaidi ya kulazimika kufanya kazi kwa bidii ili pengine bosi wangu anione anipandishe cheo ama kunipa nafasi ya kwenda kujiendeleza kielimu. Lakini tatizo kazini kwetu kumejaa majungu mno kiasi kwamba uchapakazi wangu unanifanya nionekane kimbelembele. Kila mtu ananiona nina kiherehere hadi nalazimika kuwa mpole na goigoi kama wafanyakazi wengine. Kwa mtindo huu sijui ni lini nitafanikiwa kimaisha.

Mpenzi, kweli kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu, sitamani wala siombi uniache na kuolewa na mwingine kwa sababu tu ya hali yangu duni. Machozi yananitoka mno kuyaandika maneno haya. Ninakuomba mpenzi wangu univumilie walau kwa mwaka moja mwingine pengine serikali itatufikiria na kuamua kuboresha hali zetu. Chonde chonde mpenzi wangu.

Mpenzi wangu, najaribu kukwepa kuufikiria mtihani mkubwa unaokukabili kwa sasa. Mapenzi ya kweli ama maisha bora. Najaribu tu kupambana na wivu moyoni mwangu. Najaribu kutamani kuvivaa viatu vyako na kuchagua mapenzi ya kweli. Lakini sipungukiwi imani.

Mpenzi wangu, najua nimekuchosha kwa barua ndefu sana ambayo hata hivyo imeshindwa kujibu swali lako la nitakuoa lini. Ninatumai maelezo yangu pamoja na kutojibu moja kwa moja swali lako, angalau yametoa mwelekeo wa jibu.

Mpenzi wangu, natamani kusema mengi sana zaidi ya haya. Najua hata siku moja dau tupu haliendi joshi na maneno matupu hayajengi nyumba. Ninaloweza kukwambia ni kuwa ninakupenda mno, daima ninakuwaza wewe kwa kuwa umetamalaki moyoni mwangu. Wewe ndilo pambo la moyo wangu. Kwa huba na mahaba yajazayo vibaba na vibaba, penzi langu kwako limeshiba.

Nikupendaye daima,

Mpenzi wako.

Tunapowahubiria injili wenye njaa

$
0
0

Chifu Thomas Marealle (Juni 12, 1915 – Februari 14, 2007) Mangi Mkuu wa huko Uchaggani  wakati fulani mwaka 1957  alipata kusema, "Huwezi kuhubiri injili kwa watu wenye njaa". 

Kwa hizi siku mbili nimesoma mtandaoni watu wengi wakiwaponda wanafunzi wa UDSM wanaosemekana kufanya vitendo vya ngono ili waweze kujikimu kimaisha kutokana na ugumu wa maisha unaosababishwa na ukosefu wa mikopo kwa wakati ama kukosa kabisa.

Badala ya kuwaponda, ninadhani ingependeza tungewaambia wanafunzi hawa wafanye nini ili waweze kujikimu maisha nje ya utegemezi wa pesa za serikali (inawezekana siyo zao).

Sijui nani anayeweza kusema kwa maisha ya hapa Dar es Salaama utaweza kuishi vipi pasipo pesa?  Natamani awepo mtu awaambie dada zetu na watoto wa ndugu zetu wafanye nini ili waweze kumudu kusoma na kutafuta pesa kwa njia bora zaidi.

Sikusudii kuwatetea wanafunzi hao.  Lakini nakusudia kuziambia mamlaka zinazohusika zinapaswa kuguswa na uzembe (neno baya?  basi niseme kutojali kwake) unaopelekea wanafunzi hao kutafuta mabadala wa namna ya kujikimu.

Ni aibu kubwa sana.  Sitaki kusema ni aibu kwa wanafunzi hao.  Bali nataka kusema ni aibu kwa taifa ambalo baada ya muda mfupi litakuwa na viongozi waliosoma kwa biashara ya ngono.  Viongozi watakaosimama kwenye majukwaa na kuiambia jamii juu ya maadili na tabia zenye kupendeza. 

Taifa hilo litakuwa ni zao la taifa lisilojali.  Litakuwa ni zao la taifa lililoshindwa kufahamu vipaumbele vyake vya msingi ni nini.  Litakuwa taifa la kipekee sana.  Litakuwa ni taifa lililotokana na taifa lililoona serikali haina fedha za kutosha kutatua matatizo ya wanafunzi ilhali taifa hilo hilo lilikuwa na pesa za magari ya anasa na posho za kufuru kwa walioshika mipini.

Sitamani kuyasema haya.  Lakini nisichokitamani zaidi, ni kuwa mnafiki.

Ukiyatazama maisha ya wanafunzi wengi wa elimu ya juu, utasikitika sana.  Lakini jamii hailioni hilo kama tatizo.  Tatizo kubwa linaloonekana ni wanafunzi kuishi maisha ya anasa na kujaza music systems vyumbani mwao (huu mjadala ulisumbua sana kwenye gazeti la Rais mwaka 2005 na 2006).  Tunasahau (ama tunajua ukweli ila tunauficha) kuwa wanaoishi maisha ya anasa ni wachache katika wengi wa wanafunzi wa elimu ya juu.  Kuna wachache wanaotoka familia zenye uwezo, wachache wenye ajira zao, na wachache wenye biashara zao.

Lakini sehemu kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu ni watoto wa Watanzania masikini kabisa.  Tena wengi wao wamekuja mjini kwa sababu ya elimu tu.  Hawa ni Watanzania ambao wakikosa fedha kutoka serikalini, maisha yao hayaelezeki.

Hawa ni Watanzania wanaolazimika kukomunika (kushindia chai na mkate), ambavyo pia vina gharama zake.  Hata hiyo akiba kidogo inapomalizika, nini kinategemewa?

Mimi nadhani, badala ya kuandika mitandaoni na pahala pengine tukizilaani tabia za wanafunzi hawa, tungekumbuka kuziamsha mamlaka zinazohusika ziyatazame mambo haya kwa kina kwa macho yote na kuchukuwa hatua stahiki katika kutatua matatizo ya wanafunzi hawa.

Wizara ya Elimu na idara za serikali hususani Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu amkeni jamani.

Nirudie kuazima maneno ya Mangi Mkuu Marealle kuwa hatuwezi kuhubiri injili kwa watu wenye njaa.

Ahsanteni kwa kunisoma.

Fadhy Mtanga,

Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mei 25, 2012.

Nani kasema wanaume hawana kumbukumbu na matukio?

$
0
0

Soma hii......

Mwanamke kashituka kutoka usingizini usiku wa manane na kugungua mumewe hayupo kitandani.

Mwanamke akachanganyikiwa na kuamua kushuka hadi chini.  Akamkuta mumewe ameketi juu ya jikoni, kikombe cha kahawa kikiwa mbele yake huku akionekana kusononeka sana.  Mwanamke akamtazama mumewe aliyekuwa akijaribu kujifuta machozi.

"Mume wangu una tatizo gani?" Akamwuliza huku akimsogelea.  "Kwa nini upo huku usiku wote huu?"

Mumewe akauinua uso wake.  Akamtazama.  Kisha akamwuliza, "Unakumbuka miaka 20 iliyopita tulipokuwa tumeanza kuwa wapenzi tukiwa na umri wa miaka 17 tu?"

"Nkumbuka sana mume wangu.  Jamani you are so sweet umenikumbusha mbali."  Mwanamke akajibu huku akiubusu mkono wa mumewe.

"Unakumbuka jinsi baba yako alivyotufuma kwenye siti ya nyuma ndani ya gari langu?"  Mwanaume akauliza kwa sauti ya tuo.

"Nakumbuka sana mume wangu!" Mwanamke akajibu huku akiketi sambamba na mumewe.

Mwanaume akaendelea kuongea.  "Unakumbuka baba yako alivyonioneshea bastola yake kichwani mwangu na kuniambia aidha nikuoe, ama anipeleke jela miaka 20?"

Kwa sauti ya upole mwanamke akajibu,  "Nakumbuka sana mume wangu.  Tumepitia mengi mpenzi."

Mwanaume akanywa funda moja la kahawa.  Kisha akaongea.  "Leo ningekuwa natoka zangu jela.....na kuwa huru mtaani!"

 

Chanzo: Funny Jokes  Tafsiri ya Kiswahili ni yangu.

Porojo la leo: Muungano huu si halali

$
0
0

“NDUGU yangu tizama unakokwenda…..vile vile ukumbuke ulikotoka….hii dunia…dunia uwanja wa fujo…mwenye ngoma zake acheze zipasuke….ndugu yangu tizama unakokwenda….vile vile ukumbuke ulikotokaaaaa…….”  Nashitushwa kutoka usingizini na mlio wa simu yangu.  Kitu muziki mnono kutoka kwa nguli wa muziki hayati Marijani Rajab enzi zake za Dar International.  Nakwambia mliozaliwa kizazi hiki muziki wenu ni “nana na nini” sijui na nini maneno wala hata hayaeleweki.  Muziki zamani bwana.  Hapa unakuta Mbaraka hapa Marijani hapa Chidumule hapa sijui nani na nani nimezeeka mno hadi nimeanza kupoteza kumbukumbu aisee.  Unachezea kula chumvi nyingi wewe!

Basi kabla sijaipokea simu natazama saa yangu ya ukutani.  Hii saa rafiki yangu niliinunua baada ya kutoka kwenye vita vya kumng’oa nduli.  Saa kumi na moja unusu alfajiri.  Kheee! Simu gani asubuhi asubuhi hii.  Haraka haraka nikaanza kuwafikiria wanaonidai wote.  Nikajua hapa nakumbushwa deni ukizingatia leo ni mwisho wa mwezi.  Hawa nao.  Wanakuwa kama hawajui samtaim mshahara unachelewa.  Hata hivyo nikainyanyua simu kivivu kweli.  Kutazama jina la mpigaji…..nikashituka kweli kweli.  Kumbe ni yule rafiki yangu Mzenziberi mwenye maneno chungu mbovu pasi breki utadhani nini sijui.  Mara nikajikuta dhamira yangu ikinisuta kabla hata sijapokea simu hiyo.  Toka vurugu zitokee visiwani sikumpigia walau simu kumjulia khali na salama yake.  Nikaonaje nishai.

Nikaipokea.  Akanisalimia haraka haraka.  “Salamun alaykum…”

Sauti yake inanifanya niitikie kwa hofu nyingi.  “Wa alaykum salamu wa rahmatu Allah wa barakatuh!”

Kimya kikatawala kwa nukta kadhaa.  Nikayasikia mapigo ya moyo wake yake yakidunda kwa nguvu.  Ikanipasa kuhoji.  “Kwema ndugu yangu?  Naona alfajiri mno.”

“Si kwema kaka.  Nimetoka swalaa al-fajir nikaona ninene nawe kidogo wahka moyoni mwangu upungue.  Unajua weye bwana wajua kunipa faraja wakti wa mushkeri na mitihani.”  Akaongea kwa unyonge.

Nikajaribu kuhisi kinachomzonga.  Nikaona nisipate taabu madhali mwenyewe yupo.  Nikahoji.  “Nini taabu sheikh wangu?”

Akanijibu.  “Haya mambo ya muungano haya kaka.  Muungano umekuwa dungano na myukano sasa.  Sisi na polisi.  Polisi na sisi.  Huku Unguja hakukaliki wala hakulaliki.  Ni mtafutano mtupu.  Sisi tushachoka na haya mambo sasa.”

“Mmechoka na nini?”  Nikajaribu kuuliza kwa sauti ya tuo.

“Tumechoka na muungano.  Ninyi wabara chukueni Tanganyika yenu nasi tubaki na Unguja yetu.”

“Alaa kumbe! Na vipi kuhusu Pemba?”

“Pemba tunabaki nao sisi.”

“Sawa.”  Nikameza kwanza mate.  Kama ujuavyo mate ya asubuhi yalivyo machungu.  Nikaendelea. “Kwa nini hamuutaki muungano?”

Akanijibu haraka haraka.  “Kwa mjuvi wa sheria kama wewe tena uliyeketi darasani ukazisoma hupaswi niuliza swali kama hilo.  Wewe unajua kabisa kuwa huu muungano si halali hata kidogo.  Muungano umefanyika kwa hila tu.  Sasa tunataka tupige kura halali ili tuamue hatma ya nchi yetu ya Kizanzibari.”

“Ni kweli uyasemayo.  Lakini hebu ndugu yangu tuwache mambo ya sheria kando.  Unajua tatizo sheria ipo veri tekniko.  Tulijadili hili jambo kwa akili ya kawaida tu ndugu yangu.”

“Ushaanza mambo yako.  Unataka kunitongoza kwa maneno.  Nakujua vema mwananchi wewe!  Bora hata usingesoma.  Unatumia elimu yako kudanganya tu watu.”

Makubwa leo.  Ukiona siku umeanza kushambuliwa alfajiri kama hii bora hata umdanganye bosi wako ili usiende kazini maana ni dalili hii ni siku ya shuruba kwako.  Nikajitahidi kuwa mpole na kumwuliza maswali kwa utaratibu tu.  “Basi usijali.  Tujadili kama ikupendezavyo.  Kwa nini unasema muungano si halali?”

“Muungano huu haukufanywa kwa ridhaa ya wananchi kabisa kabisa.”  Akasema haraka.

“Ni kweli kabisa.  Unadhani ridhaa ya wananchi inapatikana kwa njia zipi?”  Nikauliza.

“Kwa kura halali ya wananchi.”

“Nikuulize swali ndugu yangu kwa nia njema kabisa.  Hivi ni lini palipigwa kura ya maoni visiwani kuamua kuwa yafanyike mapinduzi ya Januari 12?”

Kimya kikatawala.  Nami nikaendelea.  “Kwa ufahamu wangu mdogo, kura halali ni zile za Disema 1963 ambazo kimsingi ndizo zilizoipa Zanzibar uhuru.  Unajua kwa nini mapinduzi yakafanyika dhidi ya serikali iliyowekwa kwa mujibu wa sheria?”

Akanijibu.  “Kwa sababu hapakuwa na namna nyingine zaidi ya mapinduzi.”

“Sawa sawa sawia.  Vivyo hivyo kwa muungano.”

“Unamaanisha nini?”

“Hata muungano ulikuwa muhimu mno.  Hapakuwa na namna ya kufanya. Mkataba ukataka pawepo na ridhio la mabaraza ya uwakilishi kwa pande zote mbili.  Bara ikafanyika.  Kwenu haikufanyika. Lakini baada ya mapinduzi yenu sheria ipi ilikuwa ikiongoza nchi?”

“Amri ya Rais.”

“Alaa kumbe! Sasa kwa nini maamuzi ya rais juu ya muungano mnayaona si halali? Lakini tawala iliyowekwa na wakoloni na mipaka iliyowekwa na wakoloni ndiyo mnayoiona halali?  Ina maana sisi Waafrika hatuna vitu vya kujivunia tulivyovifanya wenyewe hadi viwe vimefanywa na wazungu?  Ndugu yangu, unataka kuniambia mipaka iliyowekwa na wakoloni ni halali zaidi na tunapaswa kuipigania hadi kuchoma makanisha?  Kweli jamani?”

Akawa kimya.  Siku zote yeye ndo fundi wa kuongea.  Leo wacha nami niubwabwaje.  “Hebu niambie maalim wangu.  Wakoloni walipoketi Berlin pale Novemba 1884 hadi Februari 1885 wakachora kwenye makaratasi wakasema wewe Mwingereza nenda Kenya, wewe Mjerumani nenda pale Karl Peters alipopaita Deutsch-Ostafrika, na yule sultani kwa kuwa tumesumbuana sana na Waarab kwa miaka mingi toka enzi za Crusades basi tumwachie vile visiwa.  Wazungu wakaamua kitu ambacho baada ya miaka mia ishirini na kitu watu tunachomeana hadi nyumba za ibada kukipigania.  Hayo maamuzi ya wazungu yalipigiwa kura ya maoni kuamua uhalali wake?”

“Hapana sheikh!”  Akanijibu kwa kujilazimisha.

“Tunayo mambo ya msingi ya kuyapigania.  Muungano ndiyo unaosababisha maisha yawe magumu kiasi hiki?  Ndio unaosababisha bei ya sukari kutoshikika?  Kwa nini tusikae kwa pamoja na kurekebisha kasoro zilizokuwepo katika huu muungano ili uwe wa kujivunia kwa watoto wetu na vizazi vijavyo?  Haya nyie kama mnataka nchi yenu chukueni.”

“Mwananchi wewe tusiende hivyo basi.  Tujadiliane basi tuelewane. Ninyi nasi ni ndugu kabisa.  Tumeoleana tumezaliana lukuki.”  Rafiki yangu akaongea kwa upole.

“Tuje kwenye hili la juzi.  Kwa nini mnachoma makanisa?”  Nikamhoji.

“Unajua wakristo wana hila mno.  Wanafanya hila kujipanua huku Unguja ili wawe wengi?”  Akanijibu.

Nikamtwanga swali.  “Kwa nini wewe ni Mwislamu?”

“Kwa sababu namwamini Mungu Ash hadu An Laa Ilaha Ila Alah, Ash hadu ana Mohammadan Rasoul Allah.”

“Ni kweli kabisa ndugu yangu.  Lakini ngoja nikwambie kwa mtazamo wa kesukyula.  Kwa falsafa ya kawaida kabisa ya maisha.  Wewe upo dini hiyo na mwingine yupo dini nyingine kiajali tu.  Hukufanya uamuzi wewe unapozaliwa uwe dini gani.  Hata mababu wa mababu zetu waliangukia Uislamu kwa kuwa Waarabu walitawala eneo hilo kibiashara.  Wengine wakaangukia Ukristo kwa kuwa Wamishenari walitawala kibiashara eneo hilo.  Wote Waarabu kwa Wazungu walikuja kufanya biashara.  Tena wote walifanya biashara ya kinyonyaji.  Wakatubadili na dini zetu ili watunyonye kirahisi.  Tuwe na mioyo ya ‘hewala bwana’.  Wakafanikiwa sana.  Wakafanikiwa kutuachia hata chuki dhidi ya watu wasioamini kama tunavyoamini sisi.  Niambie aya ya sita ya Surat al-Kafirun inasemaje?”

“Ninyi mna dini yenu, nami nina dini yangu.”  Akanijibu.

“Sasa kwa nini tugombane ndugu yangu?  Kwa nini tuhasimiane kiasi tushindwe kuzikana?  Dini ni falsafa inayohusu mawasiliano na uhusiano wako baina yako na Mungu unayemwamini.  Dini ya mwingine isikupe taabu maana kila mtu ana kiyama chake pasi kujali ameamini nini.  Sisi ni wamoja.  Tuzijadili tofauti zetu katika hali ya kuleta mwafaka wala si katika kuleta mafarakano baina yetu.”

“Ni kweli kabisa sheikh wangu!”

“Tuna mambo mengi ya kuyafanya badala ya kupoteza muda tukigombana.”

“Ni kweli kabisa mwananchi wewe.  Naomba nikuage sheikh wangu naona simu yangu imetoa mlio wa salio kukaribia kwisha.  Niwie radhi kukuamsha usingizini lakini najua nyie watu wa Dar huu ndo muda wa kujiandaa kupambana na mafoleni.  Lakini simu yangu haijenda bure maana nimepata darasa leo.  Panapo majaliwa nitakupigia adhuhuri.”

“Insha-Allah!”

Simu ikakatika.

Viewing all 76 articles
Browse latest View live