Quantcast
Channel: Fadhy Mtanga
Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Porojo la leo: Wenyewe si mnataka kusaidiwa

$
0
0

TARATIBU Mwananchi mimi nairekebisha tai yangu.  Kisha nikaingia zangu mgahawani.  Jua linawaka vibaya mno utafikiri limeunganishwa gridi ya taifa.  Haaa!  Nilishasau humu Jamhuri ya Giza hakuna tena yale makali ya gridi ya taifa.  Siku hizi mwendo ni mgao tu miaka nenda miaka rudi na bado waziri mhusika anazidi tu kula viyoyozi kuanzia ofisini hadi kwenye gari.  Tutafanyaje sasa.

Nimeingia  zangu mgahawani hapo walau nipoze koo kwa soda baridi.  Lakini hofu yangu ni kama hizo soda baridi ntazipata maana kwa huu mgao usio na sura wala miguu wala nyuma wala mbele wala mbeleko, siku hizi soda za baridi ni anasa tupu!

“Mwananchi weweeeeee!”  Mara nasikia sauti inaniita kwa vurugu kweli.  Nageuka kumtazama anayeniita utadhani ananidai.  Heee!  Kumbe ni yule yule jamaa angu wa miaka nenda miaka rudi toka tunaendesha magari ya udongo hadi sasa tumekuwa watu wazima tunajua na stress za utawala mbovu.

“Mbona unapotea hivyo mwananchi wewe?”  Uzuri wa jamaangu huyu ni kuwa akishaanza kuongea walahi vile hakupi nafasi ya kujibu maana yeye huwa anaunganisha maswali utadhani una mashine ya kujibia.

Wakati nataka kumjibu, akazidi kubwabwaja, “Mwananchi wewe punguza kuadimika ndugu yangu….unapotea utadhani umesingiziwa kuzaliwa!”

Nikaangua kicheko.  Kisha nikairekebisha tai yangu.  “Mwananchi wewe tai yako baabkubwa sana ulinunua kwa wamachinga wa wapi?  Najua ni kwa wamachinga tu maana wewe kwa ubahili wako hauna jeuri ya kwenda kununua dukani.”

Watu wengine nao!  Isingekuwa ni rafiki yangu wa toka nitoke nakwambia Aki ya Ngai vile ningemporomoshea mvua ya matusi…maana watu tuna mastress yetu still yeye analeta makuzi.

“Tusalimiane kwanza maana unaongea tu.”  Nikaona nimtolee uvivu.

“Kwenda zako wewe!  Kwanza hebu ninunulie soda mwananchi wewe!”  Nikaona ishakuwa taabu tupu.  Kumbe mbwembwe na makelele yote hayo utadhani stendi ya Ubungo ni kutaka ofa ya soda tu hana lolote.

Nikaamua leo nami nimtolee uvivu, “We bwana wewe!  Kila siku tukikutana lazima uniombe ofa mbona wewe huwa hunipi ofa hata siku moja?”

Akaurekebisha vizuri mkanda wa suruali yake.  Alipokuwa na hakika namsikiliza, wacha aubwabwaje.  “Kwenda zako wewe…unaona ubahili kunipa ofa ya soda unanisimanga weee!  Unakuwa kama Waingereza bwana!”

Heee!  Kulikoni tena, Waingereza wamekujaje hapa?  Ikanibidi kumwuliza, “Waingereza wamekujaje hapa?”

Jamaangu akaamua kufunguka huku mate ya hasira yakimtoka mdomoni, “Nyie Watizedi hovyo kabisa.  Mmezowea kuomba omba mno misaada kwa wazungu.  Sasa kudadadeki safari hii wamewaweza!”

Nikauliza maana sipendi mafumbo mie, “Wametuwezaje?”

“Kalaghabaho!  Kumbe hujui Pinda wao Uingereza kasema msiporuhusu ushoga hampewi tena misaada!”

Kichefuchefu kikanivagaa ghafla…ama pengine nimesikia vibaya.  Nikahoji, “Unasema turuhusu wale wanaume wanaoruhusu kupumuliwa migongoni ili tuendelee kusaidiwa na wazungu?”

Jamaangu akanitizama kwa bezo.  Halafu akaongea, “We unaishi dunia ya wapi wewe?  Habari ndo hiyo.  Wazungu wamemind sasa wanasema ole wenu muwazuwie hampewi tena misaada.”

Nikamwuliza, “Hivi ndugu yangu kwani ni lazima tuishi kwa misaada?”

Kwa hasira akanijibu, “Usiwe pwimpwi wewe!  Nchi ya ajabu sana hii.  Madhahabu chungumbovu hadi wanayajengea maukuta kama ya Berlin.  Magesi usihesabu.  Maliasili ndo usiseme.  Bahari ipo. Mito ipo.  Kila kitu kipo lakini wanachakachua kila kitu wanaifanya nchi yetu iwe ombaomba kila siku.  Ndo maana tunanyanyaswa kwa sababu tumezidi mno kuwa ombaomba.”

Nikatulia najaribu kuyatafakari maneno ya rafiki yangu huyu wa miaka na miaka.  Hamu ya kunywa soda wala sina tena.  Hivi jamani jamani jamani kwanini lakini?  Kwanini tunakuwa ombaomba hadi tunawekewa masharti ya kipuuzi kabisa.

Jamaa utadhani alikuwa anayasoma mawazo yangu.  Akaanza kuongea, “Mwananchi wewe wala usisikitike sana.  Huna haja ya kuwaza sana maana haya mambo mmeyataka wenyewe wewe na marafiki zako.  Ndo matatizo ya kuchagua kwa kudanganywa na kofia na pilau.  Mnakuwa na viongozi hawana fokasi utadhani tutaacha kuwa omba omba?”

Sikumjibu kitu.  Jamaa akaendelea, “Najua huna jibu.  Wametushinda hata Libya, wamepigana vita zaidi ya miezi nane lakini umeme haujawahi kukatika.  Hawajawahi kutembeza bakuli kama lenu ambalo hadi limetoboka badala ya kukinga kwa faida ya wote misaada inavuja kwa faida ya wachache wanaolitembeza bakuli lao.”

Bado sikumjibu, “Huna jibu najua.  Sasa ndo ukawaambie wananchi wenzako wanaolalamika kila siku huko fesibuku, titwa, jamii foramu na kwingineko.  Waambie wasimlalamikie Kameruni wawalalamikie wanaoendekeza kuombaomba wakati sisi tuna kila kitu.”

Kusema kweli jamaa kanitibua nyongo yangu leo.  Aisee kumbe hali ndo ipo hivyo.

Nikaona nikiendelea kumsikiliza najiongezea stress.  Nikaondoka zangu bila hata kumwambia kwa heri!


Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Trending Articles