NIMEMALIZANA na Kevin Mponda kwenye kazi yake ya kiwango cha juu kabisa, Tai Kwenye Mzoga, ama kwa Kifaransa, L'aigle sur un cadavre.
Mara nyingi nimewasikia watu wengi, katika mazungumzo ya ana kwa ana, ama majadiliano mitandaoni; ya kwamba, hakuna mwandishi mahiri wa riwaya za Kiswahili za kijasusi katika kizazi hiki. Watu husema, baada ya hayati Elvis Musiba, mwandishi wa Willy Gamba, hakuna mwandishi mwingine fundi kuwahi kutokea. Wakimaanisha, fundi wa kuunda visa na matukio ya kijasusi kwa kiwango cha kuteka nadhari ya msomaji.
Nami, niliamini hivyo.
Lakini, sikuwa nimemsoma Kevin Mponda.
Jana nilipanga, kwa kuwa leo ni mapumziko, walau ningekwenda kudensi kidogo (nivunje mifupa wakati meno bado ipo!).
Haikuwa hivyo.
Nilikikamata kitabu hiki. Nikasema nikisome kidogo walau hadi saa 4 usiku hivi. Kisha, niende zangu.
Aah wapi!
Nilikuja kushituka, nakifunika kitabu chini, ikiwa saa tisa kasoro. Usiku mnene (wa manane na matisa!). Safari yangu ya kwenda kucheza muziki ilikuwa imekufa.
Kevin, ameiandika kazi hii kwa utulivu wa hali ya juu sana. Umahiri wake katika kusimulia matukio, ni wa kiwango cha juu sana (siyo cha nchi hii!)
Nilichokipenda zaidi, ni ufundi mkubwa sana wa kuunganisha kisa hiki cha kubuni na matukio ya kweli kabisa kuelekea mauaji ya kimbari ya Rwanda, mwaka 1994. Huhitajika akili ya ziada kwa mwandishi yeyote kulimudu hili.
Visa vya kijasusi. Usaliti. Mapenzi. Mambo haya matatu yamesimuliwa katika namna inayosisimua sana.
Wakati nikiendelea kusoma, mara kadhaa nilikuwa nikiitazama picha ya Kevin, ndani ya jalada la nyuma na kujiuliza. Hivi ni kweli jamaa huyu ndo kaandika hivi?
PONGEZI SANA KWAKE.
Kevin ametumia lugha fasaha ya Kiswahili. Maeneo mengine ameweka majadiliano katika Kifaransa, Kinyarwanda na Kingereza. Ameonesha umahiri mkubwa kwenye lugha zote nne (Kiswahili, Kifaransa, Kinyarwanda na Kingereza.
Mwandishi huyu anaonekana kuifahamu vyema mitaa ya Kigali na maeneo mengine ya Rwanda (usimuliaji wake unaweka bayana kuwa katu si Google Maps iliyomsaidia). Si hivyo tu, bali pia upeo mkubwa kwenye medani za kivita na mambo ya akiolojia. Niseme hivi, ni mwandishi mwenye weledi wa kutosha kwenye eneo analolisimulia.
Kama kawaida, mara nyingi katika riwaya za kijasusi, kuna wanawake wazuri mno (weka uzito kwenye neno mno; ukipenda sema hata nno!) ambao wanatumika kijasusi kama chambo.
Nilipomaliza kuisoma kazi hii, kama kawaida yangu, nikarukia Google kutafuta baadhi ya facts. Niseme tu, Kevin si tu ni msimuliaji anayesisimua, bali pia ni mwangalifu sana wa kile kinachoitwa, small small details.
Nitapenda siku moja kukutana na mwandishi huyu (juzi ilikuwa tukutane Dar, kukatokea jambo nje ya uwezo. Hatukukutana).
Wiki hii, kabla ya Novemba 30, nilikuwa na vitabu vinne vya kuvimaliza ndani ya siku nne; Bondia na Wimbo Wa Gaidi - Hussein Tuwa, Siku ya Utakaso - Beka Mfaume na hiki Tai Kwenye Mzoga - Kevin Mponda. Ratiba yangu haikuniruhusu kihivyo. Hata hivyo, nimemudu kuvimaliza vitatu.
Kwa kuwa nina weekend ndefu, nitamalizana na Wimbo Wa Gaidi kutoka kwa ka'mkubwa.
Nikirejea kwa rafiki yangu Kevin, vous êtes un écrivain incroyable. Vous êtes l'un des meilleurs.
Continuez votre bon travail.
Camarade par écrit,
Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Vendredi, 1er décembre 2017.