Quantcast
Channel: Fadhy Mtanga
Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Mambo Niliyojifunza Mwaka 2015

$
0
0


Wakati mwaka ndiyo umefika ukingoni, ninaketi chini.  Ninatafakari.  Ninajikuta ninazikumbuka vema siku 365 za mwaka 2015.  Kila siku moja, ilikuwa ni ukurasa moja katika kitabu cha 2015.  Kila ukurasa, umenifunza mambo mengi sana.  Ninayaazima maneno ya Mwanamapinduzi na Sauti ya Ghetto, Bob Marley, “What life has taught me, I would like to share; with those, who want to learn.”

Hivyo, yale niliyojifunza, ningependa kuwashirikisha; wale, watakao kujifunza.

1. Kuishi kwa malengo ni muhimu sana.  Ukiishi kwa malengo utafahamu wakati wa kusema ndiyo, na wakati wa kusema hapana.

2. Ni vema kuwajali wazazi.  Wapo wengi wanaotamani kuwa na wazazi lakini hawana.  Hivyo, kama umebahatika kuwa nao, wathamini kwa kuwa hawana mbadala.

3. Ni muhimu kuijali afya.  Katika yote uyafanyayo, jitahidi kuilinda afya yako.

4. Hakuna wakati sahihi utakaokuwa tayari.  Ukitaka kufanya jambo, usiseme unasubiri wakati utakaokuwa tayari.  Wakati huo hautofika kamwe.  Wakati ni uliopo.  Anzia pale pale ulipo.


5. Kuna tofauti kubwa sana kati ya kukata tamaa na kuacha kupoteza muda. Unaweza ukajua wewe si mtu wa kukata tamaa, kumbe ni mpoteza muda. Jifunze kutofautisha vema kutokana na muktadha wa jambo husika.

6. Hatuzaliwi na hamasa fulani. Tunajifunza kadri tunavyojizowesha kuyatazama mambo yanayotuzunguka kwa macho chanya.  Ukiweza kulitazama kila jambo kwa macho chanya, kila jambo litakuwa jema kwako.

7. Mahusiano ni jambo muhimu sana.  Mahusiano yenye afya huchochea ufanisi katika mambo mengi.  Na kinyume chake.

8. Kuna kitu kimoja tu duniani kinachoweza kubadili nafasi ya furaha. Kitu hicho ni, furaha.  Lakini kama ni pesa ndizo zikupazo furaha,  furaha yako ingali na walakini. Ingawa, wanasema, kuna tofauti kubwa unapolia ndani ya daladala, na unapolia ndani ya Range Rover.

9. Lakini, kama furaha yako inasababishwa na mtu mwingine, bado hujaipata.  Furaha yako inatakiwa iwe juu ya viganja vyako.  Huku ukifahamu kuwa, ukivibinua, basi umeimwaga.  Japo, mtu mwingine hapaswi kuwa chanzo cha furaha yako, kamwe, usiwe chanzo cha mtu mwingine kukosa furaha.

10. Maua mengi yavutiayo duniani, huchanua kutoka katika mashina yasiyovutia machoni, mengine, yakiwa yamesheheni miba. Yatazame maisha yako kwa mfano wa maua.  Usiumizwe na mashina ya maisha.  Furahia kichanuacho juu ya mashina hayo.

11. Kusikiliza muziki uupendao kila siku kunakufanya uzidi kuyafurahia maisha. Ukijenga mazowea ya kusikiliza muziki uupendao kila siku, wakati mwingine kuuigiza kuuimba, maisha yako yatajaa furaha.

12.  Kamwe, mafanikio hayatokuletea furaha.  Bali, furaha yako ndicho chanzo kikuu cha mafanikio yako.

13. Furahia wakati uliopo.  Usisubiri kusema ya kale dhahabu.  Tambua, ya sasa ni almasi.

14. Ni muhimu sana kufanya makosa katika maisha.  Kamwe, usiogope kufanya makosa katika maisha yako.  Usiogope kumkosea mpenzi wako, mzazi wako, rafiki yako, mkubwa wako, mdogo wako, jirani yako, ama yeyote yule.  Fanya makosa mengi kadri uwezavyo.  Makosa ndiyo ukamilifu wa ubinadamu wako.  Lakini, ni mwerevu tu, ayatazamaye makosa kwa macho chanya.  Makosa, ndiyo yatufanyayo kuwa imara.

15. Kuandika na kusoma mara kwa mara kunaongeza uwezo wa kufikiri.  Kunaliwaza moyo.  Kunachochea furaha ndani yako.

16. Ukiona uvivu kupika, mtu anaweza kukupikia. Ukiona uvivu kufua, mtu anaweza kukufulia. Lakini, ukiona uvivu kuandika, hakuna wa kukuandikia.  Unapoona uvivu kuziandika fikra zako ili zisomwe na wengine, kumbuka haya.

17. Unaweza kutingwa kukusanya mawe huku huioni almasi miguuni pako.  Tazama kwa macho chanya, maangavu yale yakuzungukayo.

18. Kama unataka kufeli maishani mwako, basi jaribu kumridhisha kila mtu.

19. Mara zote, watu tunaoepuka sana kuwaumiza maishani, ni wale wasiojali kutuumiza.

20. Usimlaumu mtu mwingine kwa jambo lolote maishani mwako. Jitafakari.

21. Kusafiri sana na kukutana na watu tofauti tofauti kunakufanya ujifunze mambo mengi sana na kuyafurahia maisha.

22. Jifunze kumshukuru Mungu kwa kila jambo.

23. Ingawa wanasema heri huzaliwa katika tumbo la shari, likuepukalo lina heri nawe.

Zaidi ya yote, ni vema kuishi maisha ya kumtegemea na kumwadubu Mungu pekee.


Wanasema, kuishi ni kujifunza.  Nami, naufurahi sana uanafunzi wangu.

Mwaka ndo ushaisha. Kama hukuuanika, bila shaka umeutwanga mbichi.  Nakutakia heri katika kuumaliza mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2016.  Mwenyezi Mungu azidi kukubariki.

Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
Alhamisi, Disemba 31, 2015.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Trending Articles