Quantcast
Channel: Fadhy Mtanga
Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Porojo za leo: Mei Mosi!

$
0
0

MWANANCHI mimi naamshwa kutoka usingizini kwa mlio mkali wa simu yangu ya Kichina.  Simu inalia kweli utadhani imefungwa sub-woofer.  Nakwambia ukubwa wa muziki wake usiombe mtu akupigie simu ukiwa kwenye ibada ama kikao nyeti kweli.  Unaweza tamani ardhi ipasuke walahi vile.  Naitazama simu ili kumfahamu mpigaji.  Naona namba tu.  Nani tena huyu wa kunipigia simu asubuhi yote hii wakati mie nataka kufaidi usingizi wa siku ya mapumziko.  Naamua kuipuuza.  Navuta shuka na kugeukia upande wa pili.

“Ndugu yanguuu tizama unakokwendaaaa…vile vile ukumbuke ulikotokaaaa….”  Simu inaita tena.  Najua vijana wa siku hizi hamuwezi kuufahamu huu wimbo wa mkongwe Marijani Rajab.  Nyie zenu ni hizi bongo fleva ambazo mnachezea mabinti wa watu na kuwabadili kama nguo halafu kila mkiacha mnatunga nyimbo ili muuze.  Kweli dunia imebadilika sana.  Watoto wa siku hizi adabu wala hakuna.  Kila mtu anajifanya ‘machi noo’.  Vijana ni vurugu kwa kwenda mbele.  Mambo ambayo zamani yalifanywa na wanyama sasa ndo yanafanywa na vijana wetu.  Taabu kweli kweli.

Hee!  Kumbe simu bado inaita.  Naitazama tena.  Namba siifahamu.  Naamua tu kuipokea maana itakuwa kero tupu.  “Haloo!”  Naitikia kwa sauti nzito utadhani nimekabwa na fupa la kuku wa kienyeji kooni.

“Mwananchi wewe upo?  Jamani mbona umekuwa adimu hivyo yakhe utadhani miguu ya nyoka?”  Asalaleeh!  Ni yule yule rafiki yangu wa Unguja.  Leo sijui kawaza nini kunipigia simu maana sijazungumza naye karibia mwaka.

“Asalaam aleykum maalim wangu!”

“Waleykum salaam!  Kitambo sana sheikh wangu.  Madhila gani yamekusibu hata ukapotea usisikike tena?  Hata kun’julia khali huna mpango.  Ama ndo mambo ya kamisheni hayo yanakufanya un’sahau mie?”  Keshaanza.  Si unamfahamu huyu jamaa huwa haishiwi maneno?  Sijui leo kaja na lipi maana huwa hapigi simu ilimradi tu.

“Maisha tu ndugu yangu!  Pilika zimekuwa nyingi kuliko uwezo wangu.”

“Sijawahi kukuona ukiishiwa utetezi.  Nilimiss sana maneno yako ya shombo ntu wewe!  (Hee!  Kumbe nna maneno ya shombo, hata sikufahamu, haya makubwa!)  Mambo mengi yanatokea nilitamani kukusikia ukisema!”  Walau leo anazungumza kwa vituo.

“Kama yapi ndugu yangu?”  Namwuliza maana’ke asije nitia maneno bure ilhali sikusema.

“Ina maana pilika ni nyingi hadi huyaoni?  Huoni komedi shoo mpya pale Dodoma?”

“Kuna nini kwani?  Hata sina habari!”  Namzuga maana sitaki kujadili mambo ya kunipa stress asubuhi yote hii!

“Tuyaache hayo ntakupigia siku nyingine.  Leo nimekupigia kuhusu Mei Mosi.  Vipi kuna uwezekano wa kupandishiwa mishahara kweli.  Nimesikiasikia tu tetesi.!”

Hapo ndipo aliponikuna.  Nikainuka na kutupa shuka kule.  Nikaketi kitako.  “Kupanda kwa mishahara?  Walahi vile ndugu yangu mie kichwa kinazidi kuniuma tu hapa!”

“Kwa nini kikuume?”

“Sasa kama gharama za maisha zinapanda kila siku unadhani huo mshahara ukipanda unaleta unafuu.  Hizo ni hesabu tu za kujumlisha na kutoa.  Ni sawa na una kumi halafu unajumlisha tano kisha unatoa ishirini.  Unadhani utabaki na kitu gani?”

“Sasa hapo mwananchi wewe si unabaki na deni la tano!”  Nikajibiwa.

“Ahaaa!  Kumbe unajua hesabu.”

“Unamaanisha nini hapo sasa maana nawe kwa mafumbo utadhani….”

Nikamkatisha.  “Siyo mafumbo.  Linganisha kupanda kwa gharama za maisha na kupanda kwa hicho kipato.  Maisha yanazidi tu kuwa magumu.  Pesa zimejenga uadui na mifuko yetu.  Ukiziweka tu wala hazitaki kukaa.    Yaani maisha haya full kizungumkuti!”

“Sasa unadhani nini kifanyike?”

“Mambo ya kufanyika yapo mengi!  Mi nadhani la muhimu zaidi rasilimali za nchi zilindwe vema kwa uaminifu.  Kila kitu kifanyike kwa uadilifu ili tufike mahali tujimudu kiuchumi.  Tatizo siyo mishahara mikubwa.  Tatizo ni udhibiti wa mfumuko wa bei.  Hiyo mishahara hata ikipandishwa kila siku kama mfumuko wa bei haudhibitiwi ni kazi bure tu.  Maisha yanazidi kuwa magumu sana.  Pesa inadhidi kukosa thamani.  Si umeona mwenyewe nauli zilivyopanda.  Zimepanda mno.  Sasa unadhani mishahara ikipandishwa inaleta utofauti gani wakati bei za bidhaa zote inapanda?  Sema mwenyewe usije sema mie nna maneno sana!”  Nikameza mate.

“Mmh!  Ila nalo neno maalim wangu!”

Tii ti tiii!  Simu ikakatika.  Sijui kaishiwa salio!  Nikajitupa tena kitandani na baridi hili tena!

Heri ya Mei Mosi!

Viewing all articles
Browse latest Browse all 76

Trending Articles