ILIPATA kutokea pahala fulani mumu humu ulimwenguni. Paliondokea mwanamume mmoja awaye rijali. Mwanaume huyo alisifika sana kijijini kwake kutokana na uchapakazi wake. Mwanaume huyo alijenga nyumba nzuri kweli. Nyumba hiyo ilipendeza kijiji kizima. Hata vijiji vya jirani, hapakuondokea kifani chake.
Mabinti makumi kwa makumi. Pengine mamia kwa mamia, walitamani sana kuposwa na mwanaume yule. Walizisikia sifa zake. Wengine walijionea sifa zake kwa macho yao. Alikuwa na akili nyingi sana. Minguvu nayo tele tele. Alilima mazao kwa jitihada zake zote na kuwa mfano wa uzalishaji kijijini pale.
Si punde, mwanaume huyo akaposa mwanamke katika mmoja wa wale makumi ama mamia ya wanawake waliotamani na kumendea kuposwa naye. Ilikuwa sherehe kubwa sana kijijini. Wakaalikwa marafiki, jamaa na ndugu kutoka vijiji vya jirani wapate kuwa mashuhuda wa ndoa hiyo.
Mwanamke huyo alikuwa na uzuri usioweza kufananishwa na kitu chochote. Kila mtu akamwonea gere. Hata wanawake wenzake wakakiri kuwa binti huyo amehitimu ulimbwende na umaridadi. Wakasema ni stahili yake kuposwa na mwanaume huyo. Kuna wanaume lukuki walijaribu kurusha kete zao kwa mwanamke huyo pasi na mafanikio. Wakaishia kula kwa macho huku udenda ukishindwa kuwakatika.
Siku nazo zikasogea pasina ajizi. Mwanaume yule akiwa na mwanamke ambaye sasa ndiye mkewe. Mwanamke huyo alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mumewe. Alimheshimu. Alimsikiliza. Alimjali na kumthamini pia. Mwanamke huyo akawa mwaminifu sana kwa mumewe. Ijapokuwa wanaume wengi sana bado waliendelea kujaribu kumtongonza, hawakuambulia chochote. Mwanamke huyo aliwakatalia katakata kwa kuwa alilidhika na mumewe. Awakubalie kwa lipi hasa wakati huduma zote anapewa na mumewe?
Si punde, mwanaume yule akabweteka. Akaanza kiburi na bezo kwa mkewe. Akajiona yeye ndiye yeye na hapana mwingine awaye yeyote wa kumfikia. Akaanza kumpiga na kumwumiza kupindukia. Akaacha kumpa huduma nzuri. Akaanza kumnyonya hata kile kidogo alichokuwa nacho huyo mkewe. Mwanamke wa watu akachakaa ghafla. Hali yake ikazidi kuwa duni zaidi.
Lakini jambo la kustaajabisha zaidi, mwanaume huyo akazidi kuwa mjivuni. Hakuacha kupayuka kuwa yeye ndiye yeye, hapana yeyote amfaaye mke wake. Akazidi kupayuka kuwa wanaume wengine wanaommendea mkewe wanajisumbua bure kwa kuwa kamwe, asilani abadan, hawatoweza kumpata.
Wanaume wenzake wakayasikia maneno hayo. Mkewe naye masikio yake hayakuwa likizo. Yakalidaka kila neno. Chambilecho wahenga, wanyimwa mlo, katu si maneno. Wanaume hao pamwe watu wengine wakamwambia mwanamke huyo juu ya majigambo ya mumewe.
Mwanamke huyo akafikiria sana. Kwa nini aendelee kuteseka kwa mume asiyemjali wala kumthamini ilhali kuna wanaume wengine chungu mbovu wenye nia ya kweli na mapenzi mema kwake? Kwa nini lakini? Bado mwanamke huyo hakupata jibu.
Akaendelea kufikiria kwa makini. Akapata jawabu kuwa kwa kuwa amekaa kwenye ndoa hiyo kwa muda mrefu, haikosi mumewe keshabweteka na kujisahau. Akagundua hiyo ndiyo sababu mwanaume ambaye ni mumewe wala hana muda naye.
Akaamua kumkubali mwanaume mwingine. Mumewe alipogundua akaja juu kweli. Kwa nini mkewe ampe nafasi mtu mwingine?
Bila ya woga, wala kumung’unya maneno, mwanamke wake akamjibu, “Umeshindwa kutimiza wajibu wako, wacha wengine wenye uwezo waje kutimiza.”
Basi, mwanaume yule akakasirika sana. Akaamua kumzushia mwanaume mpya maneno ya uwongo ili jamii imchukie. Pia akamfanyia visa mbalimbali ili aonekane asiyefaa.
Akasahau kuwa wema hushinda uovu.
Fadhy Mtanga,
Mbeya, Tanzania.
19 Novemba 2011.